HII NDIYO MIKOA INAYOONGOZA KWA USHIRIKINA TANZANIA...IMO MBEYA

MKOA wa Mbeya umetajwa kushika nafasi ya tatu kitaifa, kwa kuwa na makosa mengi ya jinai na mengi ya makosa hayo, yakitokana na imani za kishirikina.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele,alibainisha hayo kwenye mkutano wa Wadau wa Maabara Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, uliokuwa maalumu kwaajili ya uzinduzi wa kusimikwa kwa mtambo mpya wa Energy Dispersive X Ray Fluorescence(EDXRF), ambao ni maalumu kwaajili ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara.

Prof Manyele alisema mkoa wa Mbeya, unashika nafasi ya tatu kitaifa kwa makosa ya jinai, ukiongozwa na mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam. Lakini, kwa Mbeya hali ni tofauti, kwakuwa matukio mengi yanatokana na imani za kishirikina.

“Hapa kuna ubakaji hasa wa watoto unaohusishwa imani za kishirikina, masuala ya mauaji ya kuzika watu wakiwa hai kwa kuwatuhumu kuwa wachawi, lakini hata biashara nyingi zinazofanyika kwenye mkoa huu zinatajwa kuhusishwa sana na imani potofu za ushirikina sasa ili kupunguza kiwango cha makosa ya jinai ni lazima jamii yenyewe ibadilike” alisema.

Akizungumzia mashine ya ED-XRF, Prof Manyele alisema kusimikwa kwa mtambo huo, kutarahisisha upatikanaji wa majibu ya haraka juu ya uchunguzi mbalimbali wa kimaabara, ambapo mtambo huo una uwezo wa haraka wa kuchunguza na kutoa majibu.

Alisema mashine hiyo itatoa fursa kubwa kwa wanajamii, kwa kuwa muundo wake hautaishia kupimia vinasaba (DNA) tu, bali hata sambuli za madini ardhini, kemikali zilizopo kwenye vyakula, ardhini na kwenye maji hususani ya visima virefu na vifupi.

Aliwataka wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, kuitumia mashine hiyo itakayotoa huduma kwa gharama nafuu, tofauti na zile zilizokuwa zikigharamiwa kwa sampuli kukusanywa na kusafirishwa hadi Dar es salaam.

Akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Mbeya kwenye mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika, alisema mtambo huo umekuja wakati muafaka, ambao Rais John Magufuli amepiga marufuku usafirishaji wa mchanga wenye madini kwenda nje ya nchi.

Aliwataka wachimbaji wadogo na wakubwa kuitumia fursa hiyo katika shughuli zao kwakuwa sasa wataweza kujua sehemu iliyo na kiasi kikubwa cha madini kwa sampuli za udongo za maeneo husika kupimwa na si kuchimba kiholela kama inavyofanyika hivi sasa.

Akizungumzia masuala ya Makosa ya jinai yatokanayo na imani za kishirikina,mkuu huyo wa wilaya alikiri kuwa licha ya uwepo wa makanisa mengi katika mkoa wa mbeya hata ukalinganishwa na Taifa la Naijeria hali ya uhalifu ni kubwa ikilinganishwa na mikoa mingine.

“Tulichopanga hivi sasa kama serikali,tumeamua tukutane na viongozi wote wa dini na wadau wengine ili tukae tuzungumzie suala hili.Ukiangalia mauaji kila siku,ubakaji kila kona sasa tumeona tukae na hawa wenzetu ili wanapokuwa kwenye nyumba zao za ibaada wawaambie waumini wao kuwa Mbeya hatuangaliwi vizuri” alisema Mkuu wa wilaya.

IMEANDIKWA NA JOACHIM NYAMBO-HABARILEO MBEYA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527