MWENYEKITI WA BARAZA LA ARDHI JELA MIAKA MITATU KWA RUSHWA ILI ATOE UPENDELEO KWENYE KESI


MWENYEKITI wa Baraza la Ardhi la Kata ya Kisumwa wilayani Rorya mkoani Mara, Joseph Marwa (63), amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu ama kulipa faini ya Sh 500,000 baada ya kupatikana na hatia ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh 100,000 ili atoe upendeleo kwa mlalamikaji Johanes Nyakenge aliyekuwa na kesi ya mgogoro wa ardhi kati yake na Antony Nyiranda.

Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na Mwanasheria wa Takukuru Mkoa wa Mara, Mwinyi Yahaya ulidai mshitaki akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Kata ya Kisumwa Tarafa ya Suba, Januari 28, 2014 asubuhi katika kata ya Kisumwa aliomba na kupokea Sh 100,000 kutoka kwa mlalamikaji Nyakenge aliyekuwa na kesi ya mgogoro wa ardhi na Nyairanda katika shauri namba 12/2014 katika baraza hilo kama kishawishi cha kumpa upendeleo katika kesi yake hiyo.

Alipokea fedha hiyo Januari 28, 2014 asubuhi na kukamatwa akiwa na fedha hizo kama kielelezo na kufunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani. Upande wa mashitaka ulipeleka mashahidi matatu akiwemo mlalamikaji Johanes.

Mshitakiwa alijitetea na kuiomba mahakama kumpa adhabu ndogo kwa kuwa ni mzee na ana familia inayomtegemea, huku Mwanasheria wa Takukuru, Yahaya aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wanaopewa dhamana ya uongozi kwa kuchaguliwa na umma na kisha kutumia mwanya huo kwa kujipatia mali kwa njia ya rushwa kinyume cha viapo vyao vya kutoa haki sawa bila upendeleo kwa watu wote.

Hakimu Madeha aliungana na upande wa mashitaka na kumhukumu mshitakiwa kwenda jela miaka miatu au kulipa faini ya Sh 500,000 ambapo ndugu za mshitakiwa walionekana nje ya mahakama hiyo wakichangishana kumlipia faini na kufanikiwa kulipa faini hiyo, hivyo kumwokoa ndugu yao kwenda jela.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527