MADIWANI WA CCM WAGOMA KUENDELEA NA KIKAO KISA HAWAMTAKI MEYA

BAADHI ya madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamegoma kuendelea na kikao cha chama kilichokuwa kikiendeshwa na mwenyekiti wao, Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jafari Mwanyemba kwa kumtuhumu kwa ubadhirifu wa fedha.

Madiwani hao walitoka nje ya ukumbi wa mkutano, baada ya Meya Mwanyemba kukataa kumpisha katibu wa madiwani aongoze kikao.

Madiwani hao wanamtuhumu Mwanyemba kwa ubadhirifu wa Sh milioni 30 za mradi wa maji wa Zuzu.

Akizungumza na kwa niaba ya madiwani 47 wa chama, Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Jumanne Ngede alisema mradi huo wa maji ulilenga kuuwanufaisha wakazi wa kata ya Zuzu, lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua kutokana na kugubikwa na ubadhirifu wa fedha za mradi huo.

Ngede ambaye ni diwani wa Chamwino alisema kutokana na tuhuma hizo kumkabili Meya Mwanyemba, madiwani 43 kati ya 47 wa chama, walisaini karatasi ya kutokuwa na imani naye na kuwasilisha pamoja na barua kwa Mkurugenzi ya Manispaa wakilalamikia mstahiki meya huyo.

Kwa upande wake, Diwani wa Ipagala, Gambo Dotto ambaye alisaini barua kwa niaba ya madiwani wenzake wa chama ya kumtaka meya asiwe mwenyekiti wa kikao chao, alitaja tuhuma nyingine kuwa ni pamoja na kutumia madaraka vibaya, kushiriki katika vitendo vya rushwa, kushindwa kutekeleza majukumu yake vizuri na kuwadanganya madiwani kwa makusudi na kupandikiza chuki za uongo miongoni mwao.

“Tunachotaka sisi madiwani si kumvua umeya, bali tunataka asiwe mwenyekiti wa vikao vya madiwani wa chama katika kipindi hiki ambacho uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ukiendelea,” alisema Dotto.

Dotto alimtaka meya kwa heshima na busara asiongoze vikao, hivyo kwani akiwa mwenyekiti wa kikao, wajumbe wanaweza kupandwa na jazba dhidi yake, hawatakuwa na uhuru kujadili hoja zilizopo mbele yake na yeye mwenyewe anaweza kutumia vibaya nafasi ya uenyekiti na kuamua mambo vibaya.

Dotto alisema, madiwani hao walimtaka meya asiongoze vikao vyao kutokana na kutajwa na mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya Kalago Investment Limited mara baada ya kufikishwa polisi kutokana na kushindwa kutekeleza mradi huo, ambao ulikuwa ukisuasua, ndipo akamtaja meya kwamba wanashirikiana naye katika ubadhilifu wa fedha hizo.

Dotto alisema mradi huo umegubikwa na utata mwingi ukiwamo ya kutofuata taratibu kanuni za zabuni tangu kutangaza, kufungua na, kusaini mikataba na hadi kampuni kupewa tuzo ya zabuni hiyo, kitendo ambacho kilifanyika kwa siku moja na siku iliyofuatwa fedha zilichotwa hata kabla Kamati ya fedha haijafanyia kazi mkataba huo.

Dotto alisema madiwani wanashangaa meya huyo kwa kitendo cha kuamua kurudisha Sh milioni 30 kwa kupitia kampuni yake ya Mdegela International Co Limited na kudai risiti ya fedha hizo, wakati yeye hakuwa mkandarasi wa mradi na ametajwa tu kwamba anahusika na haijathibitika kwamba amezitumia.

Alipoulizwa na madiwani kwamba kwanini anarudisha fedha wakati anatuhumiwa kuhusika tu, Mwanyemba alidai kwamba anataka kujenga sifa nzuri ya manispaa hiyo, hivyo anaona bora arudishe fedha hizo kwa lengo la kuendeleza uelewano uliokuwa wa madiwani ndani ya manispaa hiyo.

Mkurugenzi wa Manispaa, Godwin Kunambi alikiri kupokea barua waliyoandika madiwani wa CCM na kusainiwa nao 43 na ameifanyia kazi kwa kumwandikia Meya ajibu tuhuma hizo dhidi yake ndani ya siku 5 tangu jana Februari 20, mwaka huu.

“Nilimwandikia Mstahiki Meya barua yenye kumbukumbu no HMD/CC 20/2/vol 111/77 ya Februari 20, mwaka huu, nikimtaka ajibu kwa maandishi kuhusu tuhuma hizo dhidi yake katika muda wa siku tano tangu jana,” alisema Kunambi.

Kunambi alisema anasubiri majibu ya tuhuma hizo kutoka kwa Meya na akiyapata, yatapalekwa kwa Mkuu wa Mkoa, Jordan Rugimbana kwa hatua zaidi.

Mwanyemba alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo dhidi yake, alidai kwamba yeye hawezi kuzungumza lolote kutokana na kwamba yupo ndani ya kikao pamoja viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Ajira, Kazi na Vijana, Antony Mavunde.

Kutokana na mradi huo kugubikwa na utata tangu mwanzo, Injinia wa Maji wa Manispaa, Sasala amesimamishwa kutokana na kusaini mkataba wa mradi huo, wakati kisheria mkataba huo unasainiwa na mwanasheria wa serikali ni injinia wa maji.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527