ZITTO KABWE AITAKA SERIKALI KUTANGAZA RASMI BAA LA NJAA TANZANIA

Kiongozi wa Chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali kutangaza rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria kutokana na hali ya chakula kuwa mbaya nchini.


Kauli ya Zitto imetolewa wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisisitiza utunzaji wa chakula baada ya kukagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Songea.


Agizo la Majaliwa pia limetolewa siku mbili baada ya Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba kutofautiana na Zitto kuhusu hali ya chakula ambapo Waziri huyo alisema hali ya chakula nchini ni shwari huku Mbunge huyo wa Kigoma Mjini akisema ni mbaya.


Jana, mbunge huyo akihutubia mkutano wa kampeni ya kumnadi mgombea udiwani Kata ya Nkome, Geita aliendelea kupigilia msumari kauli yake akisema, “Hali ya chakula ni mbaya, ni mbaya, ni mbaya.”


Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kwenye maghala ya Taifa na kujionea hali ya chakula nchini, ni vyema Serikali ikachukua hatua.


“Ninapendekeza Serikali ichukue hatua muhimu ya kisheria ya kutangaza baa la njaa nchini. Tamko la baa la njaa litaisaidia Serikali kupata bajeti ya dharura ya kununua chakula na kutoa uhuru kwa wakuu wa wilaya kutangaza bila woga kuwa maeneo yao yana njaa,” alisema Zitto huku akimpongeza Majaliwa kwa ziara hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527