Picha: JINSI LOWASSA ALIVYOKAMATWA NA POLISI GEITA,WAANDISHI WA HABARI KUPIGWA NA KUVUNJIWA KAMERA

Askari Polisi wakiwatawanya wananchi kwenye maeneo ya stendi ya zamani Mjini Geita ambao walikusanyika kusalimiana na Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya  Chadema Edward Lowassa

Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya chama cha demokrasia na Maendeleo( Chadema) Edward Lowassa,akiwapungia mkono wananchi wa Geita akiashiria kuwasalimia wakati alipokuwa akipita kuelekea kata ya Nkome
Msafara wa Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya Chama cha demokrasia na Maendeleo Chadema Edward Lowassa ukipita katika viunga vya mji wa Geita huku ukiwa umepokelewa na waendesha pikipiki maarufu kwa jina la boda boda
Kamanda wa polisi wilaya ya Geita (OCD) Ally Kitumbo akiwatawanya wananchi ambao walikusanyika kwenye eneo la stendi ya zamani
Msafara wa Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa Chadema Edward Lowasa ukielekea kituo cha polisi.
Baadhi ya askari wakiwa katika majukumu yao ya kikazi.
Askari wakiwa wameweka ulinzi kwenye uzio wa ngome ya makao makuu ya jeshi la polisi mkoani Geita,ambapo kulikuwa kukifanyika mahojiano ya Mhe Lowassa na jeshi hilo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita,Mponjoli Mwabulambo akikanusha taarifa ya kukamatwa kwa ,Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Edward Lowassa.
*****
Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)Edward Lowassa, pamoja na ujumbe aliokuwa ameambatana nao wameshikiliwa na jeshi la polisi Mkoani Geita kwa mahojiano ambayo yamedumu kwa zaidi ya masaa matat.

Tukio hilo limetoka wakati Lowassa akitokea mkoani Kagera ambapo alifika kwenye stendi ya mabasi ya zamani kwa lengo la kusalimiana na wananchi wakati akipita kuelekea kwenye kampeni za uchaguzi mdogo kata ya Nkome.

Tukio la kukamatwa kwa waziri mkuu huyo,lililoambatana na vipigo kwa waandishi wa habari wawili,Valence Robert wa Channel Ten na Joel Maduka wa Storm Fm ambaye pia ni mmiliki wa mtandao wa Madukaonline blog limetokea leo Jumatatu Januari 16,2017 majira ya saa 9:30alasiri eneo la stendi ya zamani ya mabasi iliyopo katika kata ya Kalangalala mjini Geita.


Lowassa ambaye alikuwa kwenye gari yenye namba T 771 DEA aina ya V8 Land cruser na wenzake ambao ni Khamis Mgeja pamoja na Profesa Balegu walikuwa wakitokea mjini Bukoba kuelekea mjini Geita kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani unaofanyika katika kata ya Nkome wilaya ya Geita vijijini.


Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema chanzo cha Lowassa kukamatwa kilitokana na yeye kusimama kisha kuzungumza na wananchi waliokuwa wamekusanyika katika stendi hiyo na kumweleza changamoto zinazowakabili ikiwemo ugumu wa maisha na ukame kukithiri hali ambayo imesabauisha baadhi ya maeneo kukumbwa na njaa.


Hata hivyo  kabla ya Lowassa kuanza kujibu kilio cha wananchi ha ,kamanda wa polisi wilaya ya Geita (OCD)Ally Kitumbo alifika eneo hilo akiwa ameongozana na askari zaidi ya kumi waliokuwa na silaha za moto kisha kumwamuru Lowassa kwenda kituo cha polisi bila shuruti.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wananchi waliamua kuandamana wakifuatilia kwa nyuma msafara wa waziri mkuu huyo mstaafu hadi kituo kikuu cha polisi wilaya ambako ghafla yalianza kufyatuliwa mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi ambao wakati huo walikwishaanza kujazana nje ya kituo hicho  cha polisi kufuatilia kukamatwa kwa Lowassa.


Wakiwa katika kituo cha Polisi wilaya na baada ya kuhakikisha wananchi wamekimbia kuokoa maisha yao ,baadaye msafara wa waziri mkuu huyo mstaafu aliyekuwa ameongozana na Profesa Balegu na Khamis Mgeja uliondoka kituoni hapo kuelekea makao makuu ya polisi mkoa wa Geita ukiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Hata hivyo mbali na polisi kurusha mabomu ya machozi na kupiga risasi za moto kuwatawanya wananchi hao,waandishi wa habari wawili Valence Robert na Joel Maduka waliokuwa eneo hilo wakitekeleza majukumu yao ya kazi ,walikamatwa kisha kuanza kushushiwa kipigo na polisi huku Maduka akiumizwa sehemu za mgongoni wakati Robert akipigwa kwa mateke sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani,mgongoni na miguuni.

Maduka na Robert waliokolewa na OCD Kitumbo aliyefika eneo ambalo walikuwa wakipokea kipigo kisha kuwazuia askari wake wasiendelee kuwashambulia waandishi hao ambao kwa wakati huo walikwishakamatwa Tanganyika jeki wakilazimishwa kuingia kituoni ili wawekwe mahabusu.


Waandishi hao walidai kuwa kitendo walichofanyiwa na polisi hao ni cha kinyama na hakikubaliki kwa vile kinavunja haki za binadamu ikizingatiwa kuwa walikuwa wakitekeleza majukumu yao bila kuvunja sheria za nchi.


"Kwa kweli nimeumizwa sana sehemu za mgongoni lakini pia kitendea kazi changu ambayo ni kamera ilirushwa kwa minajili ya kuivunja lakini kutokana na ugumu wa kifaa changu hakikuweza kudhurika sasa najiuliza hivi hii ni haki na je Tanzania kuna uhuru wa vyombo vya habari maana kama mwandishi anavamiwa eneo lake la kazi kisha kupigwa bila sababu’’,alisema Maduka.


Kwa upande wake Robert ambaye kwa sasa anachechemea kutokana na maumivu aliyoyapata kutokana na kipigo hicho alidai amesikitishwa na kitendo cha polisi kuvunja kamera yake ambayo amekuwa akiitumia kutekeleza majukumu yake na hajui iwapo jeshi hilo litamlipa au la.

Kwa mujibu wa waandishi hao wamedai wamepanga kuchukua PF3 kisha kufungua kesi mahakamani ili kudai haki zao kutokana na kitendo cha udhalilishaji walichofanyiwa.


Aidha Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita(GPC) Daniel Limbe mbali na kulaani kitendo hicho ameelekeza kwa waandishi waliokumbwa na madhila hayo kuhakikisha wanapata PF3 ili baadaye uongozi wa GPC umwandae wakili wake ambaye atasimamia kesi hiyo mahakamani.


"Nimesikitishwa na kitendo walichofanyiwa waandishi hao na nimeelekeza wahakikishe wanachukua PF3 ya matibabu ili tumwandae wakili wetu ambaye atasimamia kesi hiyo itakapofikishwa mahakamani lengo ni kuonyesha kukerwa na vitendo vya polisi vya kuwakamata na kuwapiga waandishi bila sababu wanapotekeleza wajibu wao wa kihabari’’,alisema  Limbe.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Mponjoli Mwabulambo amekanusha taarifa ya kukamatwa kwa Lowassa na kwamba walimzuia kwa ajili ya usalama na masuala mengi ambayo wamezungumzia ni jambo la ulinzi na kwamba walilenga katika suala la ulinzi wa jamii na usalama wa wao wenyewe.

“Kiswahili kizuri kwamba tulikuwa tumemzuia hatukuwa tumemkata isipokuwa tulikuwa tumemzuia ule msafara wake kwa ujumla nyuma ya kumzuia kwake lilikuwa ni suala la usalama na ulinzi kwa ujumla”,alisema Mwabulambo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527