DC SHINYANGA AKAGUA GHALA LA TAIFA



MKUU wa Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, Josephine Matiro, ametembelea ghala la kuhifadhia chakula Kanda ya Shinyanga, huku akiwataka wananchi kupuuza taarifa za uhaba wa chakula nchini.

Mkuu huyo wa wilaya alitembelea ghala hilo jana huku akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo kwa lengo la kujionea hali halisi ya akiba ya chakula na kusema kipo cha kutosha.

“Itakapofikia hatua kuwa kuna ulazima wa chakula cha msaada kwa kaya ambazo hazina kabisa zimezidiwa kwa kukosa chakula, ifahamike kuwa tunacho chakula cha kutosha kimehifadhiwa vizuri kwenye ghala letu hili,” alisema Matiro.

Akizungumzia hali ya chakula katika ghala hilo, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Shinyanga, Mary Shangali, alisema hadi sasa kanda hiyo inayounda mikoa minane ina jumla ya tani 9,146.916 na wanatarajia kupokea chakula tani 10,000 kutoka Mpanda mkoani Katavi.

“Katika Kanda ya Shinyanga yapo maghala manne yaliyohifadhi chakula ambapo ghala la Bukene lililopo mkoani Tabora kuna tani 2,898.994, ghala la Shinyanga tani 6,050.969, ghala la Kasulu lililopo mkoani Kigoma tani 196.629 hivyo kuna jumla ya tani 9,146.916,” alisema Shangali.

Alisema Juni mwaka jana Jeshi la Magereza walikuwa na tani 4,035 na walichukua tani 1,105 hivyo kubakiwa na tani 2,000 ambazo bado hawajachukua hadi sasa katika mgawo wao.

Shangali alisema kanda hiyo inajumuisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Mara, Tabora, Kigoma, Geita, Kagera na Shinyanga.

Kwa upande wake Ofisa Ugavi kutoka Hifadhi ya Kanda ya Shinyanga, Bitteme Mgabo alisema wamekuwa wakitoa chakula kwa maombi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa.
Na KADAMA MALUNDE-MTANZANIA SHINYANGA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post