MWANAFUNZI APIGWA RISASI KWENYE MGOGORO WA NYUMBA

Mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari Mringa, Vanessa Josephat [16] mkazi wa Sakina jijini Arusha amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi kichwani na walinzi wa kampuni ya ulinzi ya kifaru waliokuwa wakiwatoa kwa nguvu kwenye nyumba yao yenye mgogoro .


Tukio hilo limethibitishwa na kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha Charles Mkumbo ambaye alisema kuwa polisi inamshikilia Fabian Charles mlinzi wa kampuni ya kifaru pamoja na silaha aina ya shoot gun iliyo tumika katika tukio hilo huku majeruhi amelazwa katika hospitali ya KCMC kutokana na hali yake kuwa mbaya .


Kamanda mkumbo alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa tatu asubuhi katika eneo la sakina jijini hapa, ambapo alisema walinzi watatu wa kampuni hiyo waliokuwa wakilinda nyumba hiyo inayomilikiwa na Josephat Nehemia walitumia silaha hiyo kuwafyatulia familia inayoishi hapo ili waondoke na ndipo silaha hiyo ilipomjeruhi mwanafunzi huyo .


Taarifa zinaeleza kuwa December 21 mwaka huu kampuni ya udalali ya Marc Recorders Limited wakiwa na mabaunsa na watu wengine walivamia nyumba hiyo na kuwatoa nje wamiliki wa nyumba hiyo na kuondoka na vyombo vyao vya ndani wakidai nyumba hiyo imeshauzwa kwa , Thobias Ludovick Senya baada ya mmiliki kushindwa kulipa deni la shilingi million 3.7 alilokuwa akidaiwa na taasiai ya fedha Heritage.


Baada ya tukio hilo familia hiyo yenye watu wapatao kumi wakiwemo watoto na kichanga walianza kulala nje kando ya geti la nyumba hiyo wakipigwa na baridi kali pasipo kuwa na msaada wowote


Mmiliki wa nyumba hiyo Josephat Nehemia Ogaga alisema baada ya familia yake kutolewa nje wakati yeye akiwa safarini walikuja walinzi hao wa kampuni ya kifaru na kuanza kulinda na baada ya yeye kurejea alifanikiwa kuwaondoa walinzi hao na kuirejesha ndani familia yake akidai taratibu za kuuza nyumba yake hazikufuatwa ila kilichofanyika ni uhuni .


“Nikweli nilikuwa nadaiwa na Heritage financial shilingi milioni 3 .7 na nililipa deni na kubaki shilingi million 1.8 hivyo hatua ya kuja kuuza nyumba yangu yenye thamani shilingi million 200 kwa deni hilo ni uhuni mtupu umefanyika” alisema Nehemia


Hata hivyo siku moja baadae walinzi hao walirejea tena wakiwa na silaha za moto na kuanza kufyatua risasi ovyo ndani ya nyumba hiyo kwa lengo la kuwatisha familia hiyo ili waondoke ndani ya nyumba hiyo ambapo moja ya risasi ilimjeruhi mwanafunzi huyo kichwani ambaye amelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya matibabu


Kamanda Mkumbo amezitaka kampuni za ulinzi kutoingilia migogoro bila kufuata utaratibu kwani vyombo vyenye mamlaka ya kushughulikia migogoro kama hiyo vipo na hivyo amezitaka kampuni za ulinzi kufuata taratibu zao za utendaji wa kazi na kuacha kukimbilia maslahi yao ya kupata fedha haraka,


Mkumbo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527