BONDIA WA NGUMI ZA KULIPWA FRANCIS CHEKA AFUNGIWA MIAKA MIWILI


Leo December 30, 2016 Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBC) imetangaza kumfungia kwa miaka miwili Bondia wa ngumi za kulipwa, Francis Cheka kufuatia kitendo chake cha kugoma kupanda ulingoni kupigana na Bondia Abdallah Pazi “Dullah Mbabe”.

Pambano hilo ilikuwa lifanyike Desemba 25 mwaka huu, katika Ukumbi wa PTA Saba saba jijini Dar es salaam, lililoandaliwa na Promota Siraju Kaike kupitia kampuni yake ya Kaike Promotion.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Katibu Msaidizi wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBC), Chatta Michael amesema kuwa Kamisheni yake ilitoa kibali cha kufanyika kwa mpambano huo baada ya kujiridhisha kuwa taratibu zote zimefuatwa na mabondia wameridhia na kukubaliana na muandaaji, Ila wameshangwaza na Bondia Francis Cheka kugoma kupanda ulingoni kwa madai ya malipo wakati alishasaini mkataba na muandaaji ulioonyesha kuwa ameshachukua kiasi cha shilingi milioni tatu (3,000,000) na baada ya mpambano alitakiwa kupewa kitita chake cha milioni sita.

Amesema kitendo kilichofanywa na Cheka kinaweza kupoteza uaminifu baina ya mabondia na waandaaji wa mapambano, kujiondoa kwa waandaaji katika mchezo huo kwa kuona hakuna uaminifu na pia kinaweza sababisha uvunjifu wa amani kwa watazamaji, iwapo wataendelea kudanganywa uwepo wa mapambano hewa.

Hivyo Kamati ya utendaji ya Kamisheni hiyo iliyokaa Desemba 27, na kupitia kanuni za mchezo huo, imemkuta Bondia Francis Cheka na makosa ya kimakubaliano na kutangaza kumfungia kujihusisha kwa namna yeyote na mchezo huo na kutakiwa kupipa faini ya shilingi laki tano (500,000).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527