WAZIRI AMREJESHA YANGA KOCHA HANS VAN DER PLUIJM

HATIMAYE kocha wa Yanga,Hans-van-der-Pluijm amerejea tena kundini kuendelea na kibarua chake cha kuinoa Yanga ambako tayari alishafungashiwa virago.

Pluijm amerejea baada ya jitihada za Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuzaa matunda, ambapo aliendesha vikao na viongozi wa Yanga na kocha huyo kwa siku tatu mfululizo na hatimaye jana kocha huyo akakubali kuendelea na kazi yake ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.

Akizungumza na HabariLeo, Nchemba alisema hajaona sababu ya msingi ya Pluijm kuondoka kwa kuwa kocha huyo ameongoza Yanga kwa mafanikio makubwa na kwamba mechi zilizosalia kwenye ligi ni ngumu kwa upande wao.

“Mimi ni mwanachama hai wa Yanga, Hans kuna masuala alitofautiana na uongozi ya kiutawala, ambapo uongozi ulikuwa ukimshinikiza mwalimu, akapata hasira ndio akaandika barua ya kujiuzulu.
 
 “Lakini nimezungumza na pande zote mbili na nimeyaweka sawa, kama uongozi una mipango mingine ifuate taratibu za kumuondoa kwa kuwa kocha bado ana mkataba wa mwaka mzima na Yanga, na suala la malipo klabu itaendelea kumlipa kama kawaida,” alisema Nchemba Pluijm alitaka kuondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 124, za Ligi na kimataifa akishinda 77, sare 25 na kufungwa 22.

Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 106 za tangu mwaka jana, alishinda 66, sare 19 na kufungwa 20. Wakati Nchemba akisema hayo, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdetit alisema klabu hiyo imekataa ombi la kujiuzulu kwa Pluijm kwa kuwa haioni sababu ya kuachana na Mholanzi huyo.

Pluijm alijiuzulu mapema wiki hii baada ya kukerwa na uongozi wa klabu kuleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina bila kumtaarifu, akisema huko ni kumvunjia heshima. Kocha huyo akakataa hadi nafasi ya Ukurugenzi wa Ufundi ambayo inasemekana Yanga ilitaka kumpa baada ya kumleta Lwandamina kuwa kocha mkuu.

Lakini baada ya kuwaaga wachezaji siku moja kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Ruvu timu ikishinda 4-0, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliingilia kati suala hilo.

Waziri Mwigulu ambaye ni mpenzi na mwanachama wa Yanga, kwanza aliushauri uongozi kumrudisha Pluijm na baadaye akaenda kuzungumza na kocha huyo pia kumshauri akubali kurejea.

Baraka alisema tayari uongozi huo umemuandika Pluijm barua ya kumuomba radhi na kumuangukia arudi kazini akitakiwa kuongoza benchi la ufundi la Yanga dhidi ya Mbao Fc kesho.

Uongozi wa Yanga ulitaka kumuondoa Pluijm na wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh wote wazalendo na kuwaleta Mzambia Lwandamina atakayekuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.

Pluijm aliyezaliwa Januari 3 mwaka 1949, alikuwa anafundisha Yanga katika awamu ya pili baada ya awali kufundisha kwa nusu msimu mwaka 2014 kabla ya kubwaga manyanga na kutimkia Saudi Arabia na nafasi yake kuchukuliwa na Marcio Maximo ambaye naye alifundisha nusu msimu na kutimuliwa na Pluijm kurejeshwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527