JINSI WANANCHI WALIVYOPIGWA MABOMU LOWASSA AKITEMBELEA WAHANGA WA TETEMEKO KAGERA

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema Watanzania wengi bado hawajajua uzito, upana na athari kubwa za tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni mkoani Kagera na kuua watu 17 na kujeruhi wengine zaidi ya 440.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana akiwa ameambatana na ujumbe wake uliotembelea wananchi wa kata ya Amgema na Kashai waliokumbwa na tetemeko hilo lililokuwa na ukubwa wa kipimo cha richter scale 5.7.

Akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salumu Kijuu, Lowassa aliishauri Serikali kutumia zaidi vyombo vya habari vikiwamo vituo vya televisheni ili kuonyesha ukubwa wa tukio na athari zake ili kuwashawishi Watanzania wengi kujitokeza na kusaidia watu waliokumbwa na maafa ya tetemeko hilo.

Pia alishukuru kwa mapokezi kutoka kwa Kijuu na kuahidi leo atawasilisha mifuko 400 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba za waathirika wa tetemeko hilo.

“Poleni sana kwa maafa makubwa ya tetemeko, nimetembelea nimeona wananchi wetu wakilala nje kutokana na nyumba zao kubomoka kabisa huku wengine wakipoteza ndugu na watoto wao, hili ni janga la kitaifa tunapaswa kushikamana kuwasaidia wenzetu,” alisema Lowassa na kuongeza:
 
 “Nishauri jambo moja, hapa tumieni vyombo vya habari kuwaonyesha Watanzania athari za tetemeko hili naamini watajitokeza kwa wingi kusaidia wenzao, kwa sasa bado haijaelezwa vizuri kwa sababu michango inahitajika zaidi.

“Tumetafakari tukaona msaada muhimu utakaowezesha wananchi kujenga nyumba kwa sasa ni saruji, tunafahamu ilivyo gharama kuanza kujenga nyumba. Hivyo kesho (leo), Meya wa Manispaa ya Bukoba atakuja kukabidhi kwako mifuko 400 ya saruji kwa ajili ya walengwa.”

Katika hatua nyingine, Lowassa, aliyegombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) 2015, alisikitishwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kuwatawanya baadhi ya wananchi waliokuwa wamekusanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kashai kwa ajili ya mkutano wa mbunge wao.

Pia alishangazwa na utamaduni wa kupiga mabomu wananchi huku akihoji utamalizika lini.

“Utamaduni huu sijui utaisha lini, kwani tunajua uchaguzi ulishamalizika tunashangazwa na hivi vitendo vya kupiga wananchi mabomu,” alisema Lowassa.

Kwa upande wake Kijuu, alimshukuru Lowassa na ujumbe wake kwa kuguswa na maafa hayo na kuamua kwenda kutoa msaada huo.

Akisoma taarifa fupi, Kijuu alisema mbali na tetemeko hilo kusababisha vifo na kujeruhi watu pia limeleta athari kubwa ikiwamo majengo 2,072 kubomoka kabisa huku majengo 1,595 yakiwa katika uharibifu mkubwa.

“Majengo 9,000 yana mipasuko mikubwa, kwa ujumla janga hili ni kubwa na juhudi zaidi bado zinahitajika,” alisema Kijuu.

Naye Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Rwakatare, alisikitishwa na kitendo cha polisi kutawanya wafuasi, wanachama na mashabiki wa chama hicho waliokuwa wamejikusanya tangu saa mbili asubuhi kwa ajili ya mkutano wa mbunge.

“Mkuu wa mkoa tunajua wewe hauna tatizo na tumekuwa tukishirikiana tangu tukio hili lilipotokea, sasa nashangaa leo (jana) nilikuwa na mkutano wa mbunge ambao hata Lowassa asingeweza kuhudhuria.

“Lakini nashangaa polisi wamekuja pale Uwanja wa Shule ya Msingi ya Kashai na kutawanya wananchi kwa mabomu bila taarifa yoyote. Lakini pia baada ya kutembelea wananchi tulipanga kukutana kikao cha ndani ambacho nacho polisi wametangaza kisiwepo,” alisema Lwakatare.

Lowassa aliwasili mjini hapa jana saa 5:30 asubuhi na akiwa mjini hapa msafara wake ulikimbiliwa na baadhi ya madereva wa pikipiki na kila alikokuwa akipita wananchi walimsalimia kwa kupiga honi huku wengine wakipunga mikono.

Kutokana na hali hiyo, polisi waliokuwa kwenye magari ya wazi wakifuatilia msafara huo walilazimika kuwatawanya waendesha pikipiki hao ili wasiingilie msafara wake.

Katika ziara hiyo, Lowassa aliongozana na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja na Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Rajabu Kitimba.

Pia kabla hajaondoka mjini Bukoba alikwenda katika Msikiti wa Ijumaa mjini hapa kwa ajili ya kumpa pole mke wa aliyekuwa Katibu wa Chadema Kata ya Amgema, Hemed Rusea, aliyefariki ghafla baada ya ziara ya Lowassa katika kata hiyo.

Na ELIYA MBONEA-MTANZANIA KAGERA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527