SERIKALI YAPIGA MARUFUKU KUUZA ARDHI ZA KIMILA

 
SERIKALI imepiga marufuku uuzaji wa ardhi zinazomilikiwa kimila kupitia mikataba ya muda mrefu kwa watu binafsi au taasisi, kwa kuwa sehemu kubwa ya ardhi inayomilikiwa na vijiji kwa sasa ndio imegeuzwa shabaha kubwa ya wawekezaji wa nje na wa ndani.

Aidha, imebainisha kuwa itaweka ukomo wa kumiliki ardhi ili kuondoa tatizo la mtu mmoja kumiliki eneo kubwa la ardhi bila kuliendeleza.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wakati akihojiwa katika kipindi cha Tumetekeleza kilichorushwa na Terelevisheni ya Taifa ya TBC juzi jijini Dar es Salaam.

Alisema kuanzia sasa hakuna kijiji chochote kitakachoruhusiwa kuwasilisha maombi ya kubadili umiliki au kuuza ardhi kwa sababu yeyote ile hata kama ni kwa matumizi ya umma.

“Ni marufuku wageni au wawekezaji kwenda vijijini moja kwa moja kununua ardhi, waje kwangu au wapitie Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tutawapa ardhi haraka wawekeze,” alisisitiza Lukuvi.

Lukuvi ambaye alionesha kusikitishwa na tatizo lililokithiri na la muda mrefu la migogoro ya ardhi nchini, alisisitiza kuwa uamuzi wa kusitisha kuuzwa kwa ardhi hizo, pia ni njia mojawapo ya kupunguza migogoro hiyo.

Aidha, alisema bado Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kuwafanyia tathmini wawekezaji wanaomiliki maeneo makubwa ya ardhi na kushindwa kuyaendeleza na kuwatangazia kiama kwani Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia.

“Wawekezaji wanaohodhi ardhi tu bila kuitumia muda wao umekwisha, Rais John Magufuli ameshaagiza na tunalifanyia kazi. Ardhi hizi lazima tuzichukue na kuwapatia wengine,” alisema.

Alisema imebainika kuwa baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakihodhi maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya kupata mikopo kwa manufaa yao huku wananchi wengi wakikosa ardhi kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.

“Hatuwezi kuwaacha wananchi wetu waendelee kupata shida kwa sababu ya wawekezaji. Ninawaomba wananchi wajitokeze na kutusaidia kuyabainisha maeneo yote yanayohodhiwa bila kuendelezwa ili tuyarejeshe kwa Watanzania,” alisema.

Hata hivyo, alisema wizara yake itatoa mwongozo kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji kupata ardhi kwa kuzingatia mahitaji na matumizi.

“Muda wa watendaji kusababisha migogoro umekwisha lakini pia muda wa watu kuhodhi ardhi kubwa bila kuitumia nao umekwisha.”

Alisema wizara yake pia imetenga viwanja 240 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika mji wa Kigamboni na kusisitiza anayetaka viwanja kwa ajili ya kuendeleza viwanda awasiliane naye na atavipata viwanja hivyo bila rushwa wala ubabaishaji.

“Nasisitiza mtu anayetaka kujenga kiwanda popote pale aje kwangu nitampatia ardhi ndani ya siku saba,” alisisitiza Waziri huyo. Pamoja na hayo, Lukuvi alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa hawamuungi mkono kwa kuwa aliwanyang’anya ardhi zao. “Hili halitonizuia nitaendelea kuzichukua ardhi zote ambazo haziendelezwi na wawekezaji bila kujali wao ni akinanani wala uraia wao.”

Akizungumzia suala la upimaji ardhi, Waziri huyo alisema tayari Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kutekeleza mradi wa kupima ardhi nchi nzima na kwamba ndani ya miaka 10 ardhi yote itakuwa imepimwa.

“Nakuhakikishia ndani ya miaka 10, kila kipande cha ardhi Tanzania kitakuwa kimepangwa na kupimwa. Utekelezaji umeanza mkoani Morogoro kwa kushirikiana na kampuni zilizoajiliwa,” alisisitiza.

Waziri huyo, alisema lengo la upimaji huo wa ardhi ni kumuwezesha kila mwananchi awe mkulima, mfugaji, mwenye kiwanda, shamba na kila aina ya shughuli kupimiwa eneo lake ili kuliongeza thamani.

“Lakini pia sisi kama Serikali tumeanza kudhibiti bei ya upimaji ardhi kwa kushirikiana na wapimaji ardhi binafsi. Ndoto yangu ni kuifanya Sekta ya Ardhi ichangie zaidi katika pato la taifa,” alisema.

Akizungumziwa tatizo la wananchi kudhulumiwa viwanja kutokana na makosa ya watendaji, Lukuvi aliziagiza halmashauri zote nchini kuwapatia wananchi hao viwanja mbadala.

Alisema tayari wizara hiyo imeanza kutekeleza agizo katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo wananchi wote waiodhulumiwa viwanja vyao kwa makosa ya watendaji hao wameanza kupatiwa viwanja vipya mbadala.

“Lakini pia wananchi wote walioko kwenye makazi holela tutawapa heshima ya kushirikiana nao na kuwapimia ardhi ili wafaidike na makazi yao na kulipa kodi,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni, alisema bado mchakato wake unaendelea na wizara hiyo imekuwa ikipokea mawazo ya wadau mbalimbali kuhusu ujenzi wa mradi huo ambayo inayapokea na kuyafanyia kazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527