Prof. Ndalichako -"Fedha za Field Zitatolewa Baada ya Kukamilika Zoezi la Uhakiki wa Wanafunzi"


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameeleza kuwa fedha kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo zitatolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa wanafunzi waliombewa fedha hizo toka vyuo mbalimbali hapa nchini.


Prof. Ndalichako aliyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya ucheleweshwaji wa fedha hizo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.


“Kuna zaidi ya wanafunzi 2,736 hewa ambao majina yao yamewasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya kulipwa fedha za mafunzo kwa vitendo, yakiwemo majina ya wanafunzi waliofariki na waliofukuzwa chuo,” alifafanua Prof. Ndalichako.


Aliendelea kwa kusema kuwa, kuna chuo ambacho kilituma ripoti ya wanafunzi waliofukuzwa chuo mwaka 2013/2014 lakini majina hayo yametumwa tena kwa ajili ya kupewa fedha za mafunzo kwa vitendo kwa mwaka huu.


Kutokana na kasoro zilizojitokeza katika majina ya wanafunzi wanaotakiwa kupewa fedha kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo Prof. Ndalichako amesema kuwa Serikali haitatoa fedha mpaka uhakiki wa wanafunzi wanaotakiwa kupata fedha hizo utakapo kamilika kwa vyuo vyote nchini.


Aidha, Mhe. Ndalichako amesema kuwa majina ya wanafunzi hao hewa yamewekwa katika mitandao wakitakiwa kujihakiki TCU ili kujiridhisha kama kweli ni wanafunzi na wanaendelea na masomo.


Vile vile, Prof. Ndalichako amevitaka vyuo vikuu kutoa ushirikiano kwa timu zilizotumwa katika vyuo vyao kufanya uhakiki wa wanafunzi wanaotakiwa kupata fedha hizo kwani kuna baadhi ya vyuo vimekuwa havitoi ushirikiano kwa kisingizio cha kuwepo kwenye mitihani.


Aliongeza kwa kusema kuwa, vyuo kutotoa ushirikiano kwa timu zilizotumwa kufanya uhakiki wa wanafunzi hao kutazidi kuchelewesha fedha hizo kutoka mapema.
 Na: Lilian Lundo – MAELEZO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527