MSHUKIWA wa wizi alishtakiwa Jumatatu kwa kuiba mali kutoka kituo cha polisi cha Kilimani jijini Nairobi alikozuiliwa kwa kosa jingine la wizi.
Bw Samuel Njoroge Thuo alifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Kibera Tito Gesora akishtakiwa kwa kuiba vipuri vya magari yaliyozuiliwa katika kituo hicho kama eksibiti katika kesi zilizo mahakamani.
Mahakama iliambiwa kuwa Njoroge alitenda kosa hilo mnamo Agosti 22 mwaka huu akiwa mshukiwa wa wizi wa vifaa vya gari la Bw Samuel Mwaura.
Ilidaiwa kuwa aliiba vifaa tofauti vya magari katika kituo cha polisi cha Kilimani ambavyo ni mali ya huduma ya polisi.
“Ukiwa mshukiwa katika kituo cha polisi cha Kilimani, ulishiriki tendo la wizi wa vipuri vya magari vya kituo hicho ukijua kwamba ulikuwa ukitenda makosa,” shtaka lilisema.
Hata hivyo, mshukiwa ambaye hakuwa na wakili wa kumtetea, alikanusha mashtaka na kuomba aachiliwe kwa dhamana.
Lakini Bw Gesora alimkumbusha kwamba alikuwa akikabiliwa na shtaka la lingine la wizi.
“ Utasomewa shtaka lingine la wizi ambalo lilikufanya ukamatwe kabla ya kutekeleza ulilokanusha,” akasema Bw Gesora.
Shtaka hilo lilisema kuwa mnamo Agosti 22 mwaka huu katika eneo la Kilimani jijini Nairobi, aliiba vipuri vya gari la Bw Mwaura.
Alikanusha shtaka hilo pia na Bw Gesora akamwachilia kwa dhamana ya Sh30,000 na mdhamini wa kiasi sawa.
Kesi hiyo itasikilizwa Novemba 11 mwaka huu. Aidha, Bw Gesora aliagiza akabidhiwe nakala zote za taarifa za mashahidi na karatasi ya mashtaka ili ajiandae kwa kesi.
TAFADHALI BOFYA HAPA U LIKE PAGE YETU TUKUTUMIE "HABARI" MOJA KWA MOJA KILA ZINAPOTOKEA
TAFADHALI BOFYA HAPA U LIKE PAGE YETU TUKUTUMIE "HABARI" MOJA KWA MOJA KILA ZINAPOTOKEA

Social Plugin