Na Elizabeth Cosmas,Shinyanga
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imefanya ziara ya ukaguzi wa magati ya kisasa ya kutolea huduma ya maji katika kata mbalimbali za Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi kupitia mfumo wa malipo kwa kutumia tokeni.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika Novemba 5, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, amesema magati hayo yanalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji kwa urahisi wakati wowote, kwa gharama wanazoweza kumudu, na hivyo kupunguza foleni katika maeneo ya kuchotea maji. Katopola amesema mfumo huo, unaojulikana kama Smart Water Meters, unatekelezwa kwa kushirikiana na kampuni ya E Water Services kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa manispaa hiyo.
“Lengo letu ni kuanzisha mfumo utakaowarahisishia wakazi wa Manispaa ya Shinyanga kupata huduma ya maji.
Mfumo huu ni rahisi kutumia na unaozingatia uwezo wa kiuchumi wa Mtanzania. Aidha, utatusaidia kurahisisha ukusanyaji wa mapato na kupunguza madeni, kwa kuwa mtumiaji analipia huduma moja kwa moja,” amesema Katopola.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Katopola amesema magati ya kisasa yanawekwa katika maeneo mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi, hususani maeneo yenye idadi kubwa ya watumiaji na matumizi makubwa ya maji.
Amesema mamlaka hiyo inaendelea kutathmini utekelezaji wa mradi huo ili kubaini maeneo yanayohitaji huduma hiyo na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika.
Kwa upande wake, Meneja wa Ankara na Udhibiti wa Madeni wa SHUWASA, Twalibu Abbasi, amesema mfumo huo umeanzishwa ili kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi katika upatikanaji wa maji na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya mamlaka hiyo.
Abbasi amesema mfumo wa tokeni unamwezesha mtumiaji kulipia huduma ya maji kulingana na uwezo wake wa kifedha, huku kiwango cha chini cha malipo kikiwa Shilingi 500.
“Mradi huu wa huduma ya maji kwa jamii umesaidia kupunguza changamoto zinazowakabili watumiaji na kurahisisha ukusanyaji wa mapato kwa SHUWASA. Mtumiaji anaweza kulipia maji kulingana na kiasi cha fedha anachotaka kutumia, kuanzia Shilingi 500, kisha kutumia tokeni katika mfumo huo ili kupata huduma kulingana na malipo aliyofanya,” amesema Abbasi.
Naye Makoye Emmanuel, mmoja wa wananchi wanaonufaika na mradi huo, amesema magati ya kisasa yamemwezesha kujiajiri kupitia shughuli za kuchota na kusambaza maji katika maeneo mbalimbali ya mtaa.
Amesema shughuli hiyo imemsaidia kupata kipato na kujitegemea kiuchumi.
“Kipekee, napenda kuishukuru Serikali kwa kutujengea magati haya ya kisasa, kwani yamekuwa chanzo cha ajira kwangu. Ninaweza kuchota maji na kuyasambaza katika maeneo mbalimbali ya mtaa na kujipatia kipato kwa urahisi zaidi,” amesema Makoye.
Hata hivyo, SHUWASA imewataka wananchi wanaonufaika na mradi huo kutumia maji kwa uangalifu na kutunza miundombinu ya magati hayo ili yaendelee kutoa huduma bora kwa muda mrefu.
Mamlaka hiyo inaendelea kuhimiza matumizi bora ya miundombinu ya maji kwa lengo la kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi na endelevu kwa wakazi wa Manispaa ya Shinyanga.






















TAFUTA HABARI
Social Plugin