Na Dotto Kwilasa, Dodoma
TANZANIA inatarajia kuongeza kasi ya utafiti wa rasilimali za madini baada ya kampuni ya Saudi Gold Refinery kutoka Saudi Arabia kutangaza uwekezaji wa Sh bilioni 26, hatua inayotarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo.
Uwekezaji huo unakuja wakati Serikali ikiimarisha mikakati ya kuvutia mitaji na teknolojia katika sekta ya madini, kwa lengo la kuongeza shughuli za utafiti, uzalishaji, ajira na mapato yatokanayo na rasilimali zilizopo nchini.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kampuni hiyo imepatiwa leseni tisa za utafiti wa madini, kufuatia mazungumzo ya kibiashara yaliyofanyika kati ya Tanzania na Saudi Arabia.
Amesema baada ya kampuni hiyo kuonesha nia ya kuwekeza nchini, Serikali ilichukua hatua za haraka kuhakikisha inapata leseni za awali ndani ya siku saba za kazi, kama ilivyoahidiwa, na kuendelea na taratibu za kupata maeneo mengine kupitia Tume ya Madini.
Mavunde amesema Serikali inalenga kuhakikisha leseni zinazotolewa zinakuwa kichocheo cha shughuli halisi za kiuchumi badala ya kubaki kwenye umiliki wa maeneo bila kufanyika kwa utafiti au uwekezaji.
Ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wamiliki wa leseni kushikilia maeneo ya madini bila kuyaendeleza, hali inayozuia fursa hizo kutumiwa na wawekezaji wenye uwezo wa kuyaendeleza.
Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imekuwa ikifuta leseni za wamiliki wanaoshindwa kutekeleza masharti ya umiliki na kurejesha maeneo hayo ili kupisha wawekezaji wengine wenye uwezo wa kufanya shughuli za utafiti na uchimbaji.
Amesisitiza kuwa maeneo yanayorejeshwa hayagawiwi kwa kampuni kubwa pekee, bali baadhi yake huandaliwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo kupitia programu ya Mining for Brighter Tomorrow inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki katika sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, Mavunde amesema sekta ya madini imeendelea kuonesha mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, ambapo katika kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka huu imekusanya Sh bilioni 500.2 dhidi ya lengo la Sh bilioni 351, sawa na utekelezaji wa asilimia 117.8.
Amesema kwa mwaka huu wa fedha, Serikali imeweka lengo la kukusanya Sh trilioni 1.4 kutoka katika sekta hiyo, huku uwekezaji katika utafiti na uchimbaji ukitarajiwa kuwa miongoni mwa vichocheo vya kufikia lengo hilo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Saudi Gold Refinery, Faisal Suleiman, amesema kampuni hiyo imepanga kuwekeza Sh bilioni 26 katika shughuli za utafiti na uwekezaji wa madini nchini.
Ameishukuru Serikali kwa kuwapa nafasi ya kuwekeza Tanzania, akieleza kuwa kampuni hiyo inalenga kushirikiana na Watanzania katika kutekeleza shughuli zake.
Suleiman amesema uwekezaji huo unatarajiwa kutoa fursa za ajira kwa wazawa na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na sekta ya madini.
Uwekezaji huo unaweka matarajio mapya katika sekta ya madini, hasa katika kuongeza utafiti wa maeneo yenye rasilimali, kuvutia mitaji ya kimataifa na kuhakikisha uwekezaji unaochochea uzalishaji pamoja na manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania.

TAFUTA HABARI
Social Plugin