Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDEJEMBI AELEKEZA BILIONI 8.4 KUKAMILISHA UJENZI STENDI YA NAMTUMBO


Na: OWM - TAMISEMI, Namtumbo - Ruvuma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amepongeza ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Stendi ya Mabasi ya Wilaya ya Namtumbo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 8.4, huku akisisitiza usimamizi imara wa fedha hizo ili kuwanufaisha wananchi wa Namtumbo kama ilivyokusudiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo Novemba 11, 2026, akiwa Namtumbo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua mradi huo wa kimkakati, ambao ukikamilika utaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa wilaya hiyo.

“Nawapongeza kwa kuanza ujenzi wa mradi huu wa stendi, lakini imarisheni usimamizi kwani tunataka fedha hizi zilizoletwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kila senti itumike katika ujenzi kama ilivyokusudiwa,” amesisitiza Mhe. Ndejembi.

Ili kuhakikisha mikataba ya miradi ya maendeleo inatekelezeka, Mhe. Ndejembi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuzingatia uhalisia na upatikanaji wa fedha wakati wa kusaini mikataba na wakandarasi, ili kuepuka changamoto za kuongeza muda wa utekelezaji wa mikataba au kushtakiwa mahakamani na wakandarasi, huku akishauri mkataba wa ujenzi wa stendi ya Namtumbo uwe wa miaka miwili badala ya mmoja, kutokana na uhalisia wa kazi hiyo.

Akipokea maelekezo hayo kwa niaba ya Wakurugenzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema amepokea maelekezo ya kuzingatia uhalisia wakati wa kuingia mikataba na wakandarasi na kumuahidi Mhe. Ndejembi kuwa ushauri huo ni somo na utazingatiwa katika Halmashauri zote zinazosaini mikataba ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akitoa taarifa kuhusu mradi huo wa ujenzi wa stendi ya mabasi ya wilaya ya Namtumbo, Prof. Shemdoe amemueleza Makamu wa Rais kuwa mradi huo ni wa kimkakati na utagharimu Shilingi Bilioni 8.4, huku akiongeza kuwa Shilingi Bilioni moja imetolewa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo.

Prof. Shemdoe amebainisha kuwa kiasi hicho cha Shilingi Bilioni 8.4 kitatumika kujenga jengo la utawala, sehemu ya kuegesha magari, kituo cha polisi, fremu 300 za maduka ya biashara, jengo la mgahawa, barabara za ndani za kiwango cha zege zenye urefu wa kilomita 1 na mita 26 pamoja na vyoo vya watumiaji wa stendi, huku akiongeza kuwa mradi ulianza kutekelezwa Oktoba 1, 2026 na unatarajiwa kukamilika Septemba 29, 2027.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com