Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Askofu Mkuu wa Spiritual Pentecost Church duniani, Dk. Musa Samson Mlawi, amevitaka vyama vya siasa nchini kuweka kando tofauti zao na kukaa pamoja katika meza ya mazungumzo ili kutafuta mwafaka wa kitaifa utakaolinda amani, haki na mshikamano wa Watanzania.
Amesema maridhiano ni sehemu muhimu ya kujenga mustakabali wa taifa, akisisitiza kuwa mchakato huo haupaswi kuwa wa upande mmoja, bali ushirikishe Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini, makundi ya kutetea haki za binadamu na wadau wengine.
Dk. Mlawi ambaye pia ni Rais wa Tanzania Pastors Association (TPA), ametoa kauli hiyo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu hali ya taifa, akieleza kuwa mazungumzo ndiyo njia inayoweza kusaidia kutatua tofauti zilizopo bila kuathiri umoja wa nchi.
Amesema ni muhimu vyama vya upinzani ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT-Wazalendo, CUF na vingine kukubali kushiriki mazungumzo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kujenga makubaliano yatakayozingatia maslahi mapana ya taifa.
“Maridhiano kwenye taifa linaloendelea kama Tanzania ni muhimu sana. Ni vizuri vyama vya siasa vikakubaliana na utaratibu huu wa maridhiano, lakini ufanyike kwa namna ambayo itasaidia pande zote kukaa pamoja na kutafuta makubaliano ya mstakabali wa taifa kwa njia ya amani,” amesema.
Amesema katika mchakato huo ni muhimu kuzingatia haki za kila raia na makundi mbalimbali katika jamii, akieleza kuwa amani ya kudumu haiwezi kutenganishwa na haki.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhusisha viongozi wastaafu na wenye uzoefu wa muda mrefu katika uongozi wa nchi, akiwataja Rais wa zamani Jakaya Kikwete na aliyekuwa Waziri Mkuu, Joseph Warioba, kuwa miongoni mwa watu wenye uzoefu unaoweza kusaidia katika kujenga mwafaka.
Amesema viongozi hao wana historia ya kushiriki katika ujenzi na usimamizi wa misingi ya amani nchini, hivyo mawazo yao yanapaswa kusikilizwa wakati wa kutafuta suluhu ya changamoto zinazolikabili taifa.
“Tunapoingia kwenye maridhiano lazima tusikilize mawazo ya wazee wetu ambao wamekuwa wakiliongoza taifa kwa muda mrefu. Tuondoe mihemko, tuondoe kujihesabia haki na kujipendelea, kwa sababu tunatafuta jambo moja ambalo ni amani ya nchi na maendeleo ya taifa,” amesema.
Akizungumzia suala la mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela, Dk. Mlawi amesema suala hilo linaweza kujadiliwa katika mazingira ya mazungumzo na maridhiano, huku akisisitiza kuwa mjadala huo unapaswa kuzingatia haki za Watanzania wote.
Amesema suala la haki lisitazamwe kwa mtazamo wa mtu mmoja pekee, bali liwe sehemu ya mjadala mpana unaohusu namna ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki bila kujali nafasi yake katika jamii.
Aliongeza kuwa mchakato wa maridhiano unapaswa kuheshimu taratibu za kisheria na taasisi husika, akieleza kuwa mazungumzo yanaweza kusaidia kupunguza misuguano na kujenga mazingira bora ya kuendelea kwa taifa.
Katika hatua nyingine, Dk. Mlawi amewataka Watanzania kulinda amani na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuchochea vurugu, akieleza kuwa utulivu ni msingi wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Amesema amani inahitajika ili biashara, uwekezaji na utalii viendelee, huku wananchi wakipata nafasi ya kufanya shughuli zao za kujipatia kipato na kushiriki katika maendeleo ya nchi.
“ Amani ya nchi ni ya Watanzania wote. Tunapaswa kuilinda ili shughuli mbalimbali zinazoendelea nchini, ikiwemo biashara na utalii, ziweze kufanyika na maendeleo yaendelee. Vurugu haziwezi kutusaidia, kinachotusaidia ni utulivu, mshikamano na umoja,” amesema.
Maadili ya mtandaoni
Katika hoja nyingine, kiongozi huyo wa dini ameeleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa maadili katika jamii, akisema vitendo vya kudhalilisha watu kupitia mitandao ya kijamii vinahitaji kuchukuliwa kwa uzito.
Amesema kusambazwa kwa picha na video za faragha za watu bila ridhaa zao ni ukiukwaji wa utu na heshima ya binadamu, akitolea mfano tukio la mwanamke aliyedhalilishwa mtandaoni ambalo amesema limekuwa na athari kubwa kwa familia yake.
Amesema jamii inapaswa kukemea tabia hiyo na kuhakikisha watu wanaheshimiana, badala ya kutumia mitandao ya kijamii kama sehemu ya kuwadhalilisha wengine.
“Si vizuri kuendelea na tabia hii inayojitokeza kwa baadhi ya makundi ya Watanzania kudhalilishana na kutokuheshimiana. Kila mtu ana haki ya utu, kuishi na kuheshimiwa,” amesema.
Ametoa wito kwa Watanzania, hususan vijana, kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji na kuepuka kusambaza maudhui yanayovunja heshima na utu wa wengine.
Awali, Dk. Mlawi aliwapongeza viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali kwa mchango wao katika kulinda amani na mshikamano wa taifa, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa majukumu ya kuliongoza taifa.
Amesema viongozi wa dini wana wajibu wa kuendelea kuhubiri amani, upendo, kuheshimiana na maridhiano katika jamii.


TAFUTA HABARI
Social Plugin