
Na Mbuke Shilagi Kagera.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kurejesha Sh. 277,801,365 kupitia kesi zilizoshinda mahakamani katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 11, 2026, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Hajinas Onesphory, amesema fedha hizo zimerejeshwa katika taasisi, halmashauri, vyama vya ushirika na vikundi mbalimbali vilivyokuwa vimeathiriwa na vitendo vya ubadhilifu na rushwa.
Ameeleza kuwa miongoni mwa fedha hizo ni Sh. milioni 100 zilizorejeshwa katika akaunti ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kutoka Kampuni ya STC Construction, kufuatia ubadhilifu wa fedha za mradi wa maji katika Kijiji cha Katare, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini.
Aidha, Sh. milioni 25.8 zilirejeshwa TANESCO Kyerwa, huku fedha nyingine zikirejeshwa katika vyama vya ushirika, halmashauri na vikundi vya wananchi.
Katika hatua nyingine, amesema TAKUKURU Kagera imefuatilia matumizi ya Sh. 8,984,791,617.83 katika utekelezaji wa miradi 67 ya maendeleo.
Amesisitiza kuwa wananchi na wasimamizi wa miradi wana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji ili kubaini na kuzuia changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.




TAFUTA HABARI
Social Plugin