Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZUNGU ACHAGULIWA RAIS WA MKUTANO WA 153 WA IPU


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amechaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaofanyika jijini Arusha, Tanzania.

Zungu amechaguliwa leo, Oktoba 6, 2026, wakati wa Mkutano wa Baraza la Uongozi la IPU uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), baada ya kupendekezwa na Spika wa Bunge la Wawakilishi la Uingereza (House of Commons), Sir Lindsay Hoyle. Pendekezo hilo liliungwa mkono na wawakilishi kutoka Falme za Kiarabu na Uganda, na kupitishwa bila pingamizi.

Akitoa hoja ya kumpendekeza Zungu, Sir Lindsay Hoyle amesema ana heshima kubwa kupendekeza jina la Spika huyo wa Tanzania, akieleza kuwa urafiki wa muda mrefu na wenye mizizi kati ya taasisi za mabunge ya Tanzania na Uingereza umempa sababu ya kufanya hivyo.

“Ninayo heshima kumpendekeza Spika wa Tanzania kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Naweza kusema urafiki wa muda mrefu, urafiki wenye mizizi, ndiyo maana kwa heshima kubwa nampendekeza Spika wa Tanzania,” amesema Sir Lindsay Hoyle.

Akitoa salamu za shukrani baada ya kuchaguliwa, Zungu amewashukuru wajumbe kwa kumuunga mkono na kueleza kuwa amekubali kushika nafasi hiyo kwa moyo mmoja.

“Mheshimiwa Rais wa IPU na wajumbe wote wa Mkutano huu, kwa moyo wa dhati, nawashukuru wajumbe wote. Tanzania inajivunia kuwakaribisha jijini Arusha na tutaendelea kuwa pamoja katika Mkutano huu wa 153 wa IPU,” amesema Zungu.

Kwa upande wake, Rais wa IPU na Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amempongeza Zungu kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa IPU.

Katika nafasi hiyo, Zungu ataongoza shughuli za Mkutano wa 153 wa IPU hadi Oktoba 9, 2026, wakati wajumbe wanatarajiwa kumchagua Rais mpya wa IPU atakayemrithi Dkt. Tulia Ackson.

Mkutano wa 153 wa IPU unaofanyika Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, unawakutanisha viongozi wa mabunge na wabunge kutoka sehemu mbalimbali duniani kujadili masuala ya utawala bora, demokrasia, amani, maendeleo endelevu na ushirikiano wa kimataifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com