
Mkuu wa Idara ya Taka Ngumu, Gesi, Usafi na Mazingira katika Manispaa ya Bukoba, Bw. Joseph Tambuko.
Na Mbuke Shilagi Kagera.
Mkuu wa Idara ya Taka Ngumu, Gesi, Usafi na Mazingira katika Manispaa ya Bukoba, Bw. Joseph Tambuko,ameeleza kuwa hali ya usafi wa mazingira katika Manispaa ya Bukoba inaendelea kuwa nzuri, huku juhudi za maandalizi ya mapema, ikiwemo usafishaji wa mitaro ya maji ya mvua, zikitajwa kuwa miongoni mwa hatua zilizosaidia kupunguza athari katika maeneo yanayokabiliwa na mafuriko wakati wa mvua zinazoendelea kunyesha.
Akizungumza ofisini kwake na Malunde Blog, amesema kuwa Manispaa imeendelea kuhimiza ushiriki wa wananchi katika shughuli za usafi, hususan katika kipindi hiki cha mvua kinachotajwa kuhusishwa na mvua za El Niño, ambapo utunzaji wa mazingira unahitaji kupewa kipaumbele zaidi.
Amesema kuwa maeneo ambayo kwa kawaida hukabiliwa na changamoto za mafuriko wakati wa mvua hayajaripotiwa kupata madhara yaliyotarajiwa kutokana na mvua zilizonyesha, akieleza kuwa maandalizi ya mapema yaliyofanywa na wananchi kwa kushirikiana na Manispaa ikiwemo kusafisha mitaro, yamechangia kuimarisha hali ya mazingira.
Aidha, Bw. Tambuko amebainisha kuwa Manispaa ya Bukoba ina utaratibu wa kufanya usafi kila wiki siku ya Alhamisi na Jumamosi ya mwisho wa kila mwezi, hatua inayolenga kuimarisha ushiriki wa wananchi katika kutunza maeneo yao na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Amewataka wakazi kuendelea kushiriki katika siku hizo maalumu za usafi na kuhakikisha kuwa taka zinatunzwa katika maeneo yanayostahili, huku wakiepuka kuzitupa katika mitaro ya maji ya mvua, jambo linaloweza kuzuia mtiririko wa maji na kuongeza hatari ya mafuriko.
Vilevile, amewakumbusha wananchi kuzingatia ratiba za magari ya kukusanya taka katika mitaa yao ili kuhakikisha uchafu unaondolewa kwa wakati na mazingira yanaendelea kuwa safi.
Bw. Tambuko amesisitiza kuwa jukumu la kutunza usafi wa Manispaa ya Bukoba linawahusu wakazi wote pamoja na wageni, akiwataka kila mmoja kuwajibika katika eneo analoishi, kufanyia biashara au kutembelea.
Ameeleza kuwa kuendelea kushirikiana katika usafi wa mazingira ni hatua muhimu katika kulinda afya za wananchi, kuzuia magonjwa yanayoweza kuhusishwa na mazingira machafu na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.
Amewataka wananchi kuendeleza utamaduni wa usafi hata baada ya mvua kupungua, ili kuhakikisha Manispaa ya Bukoba inaendelea kuwa safi, salama na yenye mazingira yanayovutia.
Social Plugin