Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DED MGAYA "KILA MTUMISHI AWAJIBIKE UONGEZAJI MAPATO"- KISHAPU


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Niceforous Mgaya akizungumza na watumishi wa Makao Makuu ya Halmashauri hiyo wakati akijitambulisha kwao walipokuwa kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri Oktoba 6, 2026

Na Sumai Salum-Kishapu


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Niceforous Mgaya, amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo kuzingatia nidhamu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya muda wa kazi, huku kila mmoja akiwajibika kikamilifu katika eneo lake la utendaji.


Mgaya ameyasema hayo Oktoba 6, 2026, wakati akizungumza na watumishi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo. Amesema watumishi wanapaswa kuwa makini katika utumishi wa umma, ikiwemo matumizi ya simu wakati wa kazi, mavazi na kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu zinazoongoza utumishi wa umma.


Katika eneo la ukusanyaji wa mapato, Mkurugenzi Mgaya amewataka watumishi wote kubeba wajibu wa kuhakikisha mapato yanakusanywa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, hususan katika kuboresha huduma kwa wananchi.


Amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, Halmashauri imefikia asilimia 50 ya makusanyo ya mapato ya ndani, hivyo juhudi zinapaswa kuimarishwa ili kufikia na kuvuka lengo la asilimia 100 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha. “Tusimamie vyanzo vilivyopo na kuhakikisha mwenye kulipa kodi, tozo na faini kwa mujibu wa sheria ndogo na sheria mama anafanya hivyo” amesema.


Ameongeza kuwa watumishi wanapaswa kutambua vyanzo vipya vya mapato kwa kusoma na kufuatilia nyaraka mbalimbali za Serikali, akisisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya Serikali, pia waendelee kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji na matumizi ya mapato, pamoja na kusimamia vizuri vyanzo vilivyopo na kudhibiti matumizi yasiyo na tija.


Katika utoaji wa huduma, amesema watumishi wanapaswa kusikiliza changamoto za wananchi na kuhakikisha huduma kama afya, ardhi, elimu, sheria na masuala ya utawala zinawafikia wananchi kwa wakati huku akiwataka wataalamu wa idara na vitengo kwenda kwa Wananchi kuwasikiliza, kutoa elimu na kufafanua mipango ya Serikali ili wapate uelewa sahihi wa masuala mbalimbali yanayowahusu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Niceforous Mgaya akizungumza na watumishi wa Makao Makuu ya Halmashauri hiyo wakati akijitambulisha kwao walipokuwa kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri Oktoba 6, 2026


Kuhusu miradi ya maendeleo, amewataka walezi wa Kata kufahamu miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao, ikiwemo inayofadhiliwa na Halmashauri, Serikali Kuu, wadau na wananchi, pamoja na kujua thamani, hatua iliyofikiwa na changamoto zake. Pia amewataka wanasheria wa Halmashauri kusimamia mikataba kuhakikisha Halmashauri na wananchi wanapata stahiki zao kwa mujibu wa sheria na makubaliano.


Amewataka watumishi kutokuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wanaohitaji leseni, bali wawape elimu na kuwasaidia kuelewa fursa za ubunifu na uendelezaji wa biashara zao kwani ni muhimu kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwatoa katika mazingira hatarishi kwa kuwasaidia kuwa na shughuli za uzalishaji na miradi mbalimbali ya kuwaingizia kipato.


"Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inasisitiza Serikali za Mitaa kusimamia utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia miongozo na taratibu za utendaji kazi, niwashauri katika muda wenu wa ziada mjitahidi kujenga uchumi wenu kupitia ubunifu na kuanzisha miradi binafsi, ila shughuli hizo hakikisheni haziathiri majukumu yenu ya msingi ya utumishi wa umma"Ameongeza Mkurugenzi huyo.


Kwa upande wa ongezeko la uhitaji wa baadhi ya huduma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za Walimu na kuongezwa kwa walimu wa sanaa ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma stahiki amesema Halmashauri itaendelea kuishauri serikali.


Aidha kupitia kikao hicho Mkurugenzi Mgaya anaonesha kuwa mafanikio ya Halmashauri yanategemea uwajibikaji wa kila mtumishi katika eneo lake, usimamizi mzuri wa rasilimali na kuweka mbele maslahi ya wananchi wanaohudumiwa na Halmashauri.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Josephati Limbe akizungumza na watumishi wa makao makuu ya Halmashauri hiyo Oktoba 6, 2026 kaika ukumbi wa mikutani wa Halmashauri
Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Rasilimali watu Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mona Bitakwate

































































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com