Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VETA: VYUO VIPYA 65 KUONGEZA NAFASI ZA MAFUNZO, WANAFUNZI 130,892 KULENGWA 2027



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema inatarajia kuongeza kwa kiasi kikubwa fursa za mafunzo ya ufundi stadi nchini, baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa vyuo vipya 65 vinavyotarajiwa kuanza kutoa mafunzo Januari 2027.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema vyuo hivyo, vinavyohusisha 64 vya wilaya na kimoja cha Mkoa wa Songwe, vitaongeza uwezo wa mamlaka hiyo kudahili wanafunzi wapya 130,892 mwaka 2027.

Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma jana, Kasore amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za elimu na mafunzo ya ufundi stadi karibu na wananchi na kuhakikisha kila wilaya nchini inakuwa na angalau chuo kimoja cha VETA.

Amesema ongezeko hilo la vyuo ni sehemu ya mkakati mpana wa VETA kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira, badala ya kuongeza idadi ya wanafunzi wanaomaliza mafunzo bila kuwa na ujuzi unaohitajika katika uchumi.

Kwa mujibu wa Kasore, udahili katika vyuo vinavyomilikiwa na VETA umeongezeka kutoka wanafunzi 69,347 mwaka 2022/2023 hadi 116,468 mwaka 2025/2026, ikiwa ni ongezeko lililochangiwa kwa kiasi kikubwa na kuanza kwa shughuli za vyuo vipya 33 katika ngazi za mikoa na wilaya.

Amesema baada ya kukamilika kwa vyuo vipya 65, VETA itakuwa na zaidi ya vyuo 145 nchini, ikiwamo miundombinu ambayo baadhi ya halmashauri zimekabidhi kwa ajili ya kuanzishwa kwa vyuo vya mamlaka hiyo.

Kasore amesema VETA pia itaongeza msukumo katika mafunzo yanayolenga sekta zenye mahitaji makubwa ya wataalamu, ikiwamo kilimo na uchakataji wa mazao, ujenzi, madini, nishati, TEHAMA, usafiri na usafirishaji, uzalishaji viwandani na uchumi wa buluu.

Amesema mahitaji ya mafundi yanaongezeka kutokana na kupanuka kwa uwekezaji, viwanda, miradi ya ujenzi, sekta ya madini, utalii, kilimo cha kisasa na matumizi ya teknolojia, hivyo kuna umuhimu wa kuwaandaa Watanzania wenye ujuzi unaoendana na mabadiliko hayo.

“Fursa zipo, kinachohitajika ni ujuzi,” amesema Kasore, akisisitiza kuwa ufundi stadi ni nyenzo ya kuwawezesha Watanzania kupata ajira, kujiajiri, kuunda ajira na kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi.

Katika kuimarisha ubora wa mafunzo, amesema VETA imenunua vifaa vya kufundishia na kujifunzia vyenye thamani ya takribani Sh9.596 bilioni mwaka 2024/2025 na vifaa vingine vyenye thamani ya Sh3.4 bilioni katika mwaka 2025/2026.

Amesema mamlaka hiyo pia imeandaa mitaala mipya 29, imefanyia mapitio mitaala 91 na kuboresha mitaala 13 ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira, mabadiliko ya teknolojia pamoja na mafunzo ya uanagenzi pacha na shughuli za uchimbaji madini.

Mbali na kuongeza udahili, VETA imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha ujasiriamali na urasimishaji wa ujuzi wa mafundi waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi wa mafunzo. Kupitia programu ya RPL, jumla ya mafundi 18,008 wamerasimishiwa ujuzi wao kupitia Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi.


Kwa upande wa mafunzo kwa vitendo, Kasore amesema watumishi 600 kutoka kampuni 16 walinufaika na Programu ya Kukuza Ujuzi (SEP), huku wajasiriamali 4,465 wakipatiwa mafunzo kupitia mpango wa INTEP katika kipindi kilichopita.

Amesema VETA pia imejipanga kufanya mapinduzi ya kidijitali kupitia Programu ya Elimu na Ujuzi kwa Ajira zenye Tija Awamu ya Pili (ESPJ II), ikiwamo kuanzisha Jukwaa la Kitaifa la Mafunzo ya Ufundi Stadi Kidijitali na kuandaa moduli 50 za mafunzo mtandaoni.

Kupitia programu hiyo, amesema wanafunzi 8,333 wataelekezwa namna ya kutumia mfumo wa kujifunza kidijitali, huku wakufunzi na wanafunzi 250 wakijengewa uwezo wa kuandaa na kuendesha mafunzo kwa njia ya kidijitali.

Aidha, VETA imechagua vyuo 15 kuwa Vituo vya Umahiri vitakavyobobea katika maeneo mbalimbali yakiwamo usafiri na usafirishaji, uungaji na uundaji vyuma, ukarimu, TEHAMA, kilimo na ufugaji.

Katika sekta ya madini, Kasore amesema VETA imeandaa mitaala sita ya mafunzo ya uchimbaji madini chini ya ardhi kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM), huku programu hizo zikilenga kuandaa wataalamu katika uendeshaji wa mitambo mbalimbali ya uchimbaji.

Amesema kupitia Mradi wa Madini Muhimu, vijana wapatao 400 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya uchimbaji, uchakataji na ukuzaji wa mnyororo wa thamani katika sekta ya madini.


Kasore amesema mikakati hiyo inalenga kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo VETA inalenga kuzalisha takribani wahitimu 5,635,529 wenye ujuzi ifikapo mwaka huo.

Amesema lengo la VETA si kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoingia vyuoni pekee, bali kuhakikisha mnyororo wa udahili, mafunzo, umahiri, ajira au kujiajiri, tija na uzalishaji unafanya kazi kwa ufanisi.

Amesisitiza kuwa wakati umefika kwa jamii kubadili mtazamo kuhusu ufundi stadi na kuacha kuuchukulia kama elimu ya watu waliokosa fursa nyingine za kielimu, akisema Tanzania inayolenga kuwa na uchumi wa kisasa inahitaji mamilioni ya watu wenye ujuzi wa vitendo.

“Tanzania ya viwanda inahitaji mafundi; Tanzania ya madini inahitaji mafundi; Tanzania ya TEHAMA inahitaji mafundi; Tanzania ya kilimo cha kisasa inahitaji mafundi; Tanzania ya ujenzi inahitaji mafundi,” amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com