Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Abdallah Mitawi, ameipongeza Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa mabadiliko makubwa na hatua za maendeleo iliyopiga kwa kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake, ikiwemo kuongeza idadi ya ndege hadi kufikia 16 na kupanua mtandao wa safari hadi kufikia vituo 17 ndani ya Tanzania na 20 nje ya nchi
Amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake katika Kampuni hiyo, ambapo alipokea taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu, mafanikio na mipango ya maendeleo ya ATCL
Bw. Mitawi amesema ongezeko la mapato ya Kampuni hadi kufikia takribani Shilingi bilioni 700 katika mwaka wa fedha 2025/26 ni mafanikio makubwa yanayopaswa kuendelezwa kwa kuongeza ufanisi, tija na ubora wa huduma
Ameitaka ATCL kuendelea kuwa bunifu, kutumia ipasavyo teknolojia katika shughuli zake na kuimarisha ushirikiano na mashirika ya ndege ya kikanda na kimataifa ili kuongeza ushindani, kupanua masoko na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika soko la usafiri wa anga
Aidha, Naibu Katibu Mkuu ameitaka ATCL kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa za El Nino na kuongeza kuwa kutokana na umuhimu wa usafiri wa anga katika shughuli za kiuchumi na kijamii, ni muhimu Kampuni kuimarisha mifumo ya utayari na kuchukua hatua za mapema kuhakikisha athari zinazoweza kujitokeza zinapunguzwa, huku usalama na mwendelezo wa huduma ukiendelea kupewa kipaumbele
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mha. Peter Ulanga, amesema Kampuni imeendelea kutekeleza mikakati ya kupanua mtandao wa safari, kuongeza mapato na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na mashirika ya ndege ya kimataifa ambapo hadi sasa ATCL imefikia ushirikiano na mashirika 15 ya nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza fursa za biashara, kuboresha muunganiko wa safari na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika mtandao wa usafiri wa anga kikanda na kimataifa.



Social Plugin