Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MOI YAOKOA SH121.9 BILIONI, TANZANIA YAPUNGUZA RUFAA ZA MATIBABU NJE



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Tanzania imeokoa zaidi ya Sh121.99 bilioni ambazo zingetumika kugharamia matibabu ya Watanzania nje ya nchi, baada ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, hatua iliyowezesha wagonjwa 2,282 kupata huduma hizo ndani ya nchi katika mwaka wa fedha 2025/2026. 

Mafanikio hayo yamekuja sambamba na huduma kwa jumla ya wagonjwa 211,359 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026.

Akizungumza jijini Dodoma September 1,2026 wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya MOI, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema upanuzi wa huduma, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuongezeka kwa uwezo wa wataalamu wa ndani kumeifanya taasisi hiyo kupunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi.
 Amesema hatua hiyo imepunguza rufaa za wagonjwa wa mifupa kwa asilimia 98 na wagonjwa wa ubongo kwa asilimia 97, huku huduma kama upasuaji wa ubongo, upasuaji kupitia matundu, tiba ya pingili za mgongo, upasuaji wa nyonga, uwekaji wa goti bandia na matibabu ya scoliosis zikitolewa nchini.

Kwa mujibu wa Dkt. Ulisubisya, kati ya wagonjwa 211,359 waliopata huduma, 202,000 walikuwa wagonjwa wa nje na 9,359 walilazwa.

 Aidha, wagonjwa 71,819 walipata huduma za tiba ya mwili, huku vipimo 83,847 vya radiolojia vikifanyika, vikiwemo MRI 11,533, CT Scan 6,796 na X-Ray 53,384. Alisema MOI pia imeendelea kuboresha huduma za kibingwa kupitia kliniki ya tiba ya maumivu, upasuaji rekebishi wa viungo vilivyopooza na kuondoa uvimbe wa ubongo kupitia tundu la pua.

Mafanikio hayo yameanza pia kuifanya Tanzania kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi, ambapo MOI ilihudumia wagonjwa 270 kutoka Comoro, Msumbiji, Malawi, Zambia, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Burundi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Dkt. Ulisubisya alisema mvuto huo unatokana na uwepo wa wataalamu wenye uzoefu, vifaa tiba vya kisasa na huduma za kibingwa zinazopatikana nchini, huku kiwango cha kuridhika kwa wagonjwa kikifikia asilimia 87.5 na utekelezaji wa hatua za kudhibiti maambukizi ukipanda kutoka asilimia 70 hadi asilimia 81.

Katika kuimarisha rasilimali watu na tafiti, MOI ilipandisha vyeo watumishi 199, kubadilisha kada watumishi 15 na kuajiri watumishi wapya 112, huku wataalamu saba wakipelekwa nje ya nchi kwa mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi.

 Kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), MOI imeendelea kuwa kituo cha mafunzo kwa wataalamu wa mifupa, mishipa ya fahamu, upasuaji wa ubongo, usingizi na tiba ganzi, sambamba na kuchapisha machapisho 36 ya kisayansi katika majarida ya kimataifa.

Wakati huo huo, MOI imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia huduma mkoba, ambapo wagonjwa 18,455 walihudumiwa, wakiwemo 14,145 waliopata huduma za kliniki na 4,310 waliofanyiwa upasuaji.

 Taasisi hiyo pia inaendelea na miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni, ikiwemo jengo jipya la OPD la Sh13.8 bilioni ambalo limefikia asilimia 55 na kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 280, pamoja na ukarabati wa MOI Annex wenye thamani ya Sh2.1 bilioni ambao umefikia asilimia 99.

Katika hatua inayolenga kupanua zaidi huduma, Dkt. Ulisubisya alisema MOI iko tayari kutoa huduma za kibingwa kwa wanamichezo na wageni wakati wa AFCON 2027, ikiwa na madaktari bingwa bobezi zaidi ya sita wa tiba za michezo, kliniki maalum kwa wagonjwa wa kimataifa, vyumba 25 vya kulaza wagonjwa na vifaa vya kisasa kama MRI, CT Scan, Cathlab, Brain Lab na Digital X-Ray. Alisema taasisi hiyo pia imepanga kujenga Kituo cha Matibabu ya Uti wa Mgongo na Urekebishaji wa Viungo Mbweni Mpiji, Dar es Salaam, pamoja na kuanzisha huduma za OPD katika MOI Annex, Upanga, na kusogeza huduma katika mikoa mbalimbali kupitia outreach na satellite centres.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com