NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Jubilee Life Insurance Tanzania imezindua bidhaa tatu mpya za bima ya maisha zinazolenga kuwasaidia Watanzania katika uwekaji akiba, maandalizi ya elimu, ulinzi wa maisha na mahitaji mengine ya kifedha ya baadaye.
Bidhaa hizo zilizozinduliwa leo Septemba 3, 2026 jijini Dar es Salaam ni Fanaka Plus, Smart Education Insurance Plan na Akiba Flex Plan.
Akizungumza katika hafla hiyo leo Septemba 3, 2026 Jijini Dar es Salaam Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Life Insurance Tanzania, Helena Mzena, amesema kampuni hiyo imeendelea kuboresha bidhaa zake ili kuwapatia wateja thamani na uhakika zaidi.
Amesema Fanaka Life Plan imeboreshwa na kubadilishwa jina kuwa Fanaka Plus, ikiwawezesha wateja kukuza fedha zao huku wakipata ulinzi wa maisha na amani ya moyo.
Kwa upande wa Akiba Flex, amesema bidhaa hiyo inawapa wateja uhuru zaidi wa kuweka michango na kufanya miamala ya fedha kulingana na mahitaji yao.
Amesema Smart Education Insurance Plan imeundwa mahsusi kuwasaidia wazazi na walezi kujiandaa kwa ajili ya elimu ya watoto wao.
“Hapa, mteja anaweza kuweka akiba ili kuhakikisha ndoto za kielimu za watoto wake zinatimia, huku pia akiwa na ulinzi wa maisha,” amesema.
Mzena amesema bidhaa hizo ni ushahidi wa dhamira ya Jubilee Life Insurance Tanzania ya kuwapatia wateja suluhisho linalozingatia mahitaji yao na kusaidia kutimiza mipango yao ya maisha.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Jubilee Insurance, Amyn Lalji, amesema uzinduzi huo ni hatua nyingine muhimu katika safari ya Jubilee Life Insurance Tanzania na unaakisi dhamira ya kampuni hiyo ya kutoa suluhisho bunifu na la vitendo linalokidhi mahitaji yanayobadilika ya Watanzania.
Kwa upande wake mwakilishi wa Kamishna kutoka TIRA, Alex Rocky amesema ubora wa bidhaa za bima haupaswi kupimwa kwa idadi ya watu waliojiunga pekee, bali pia kwa kiwango ambacho bidhaa hizo zinawawezesha wananchi kuelewa na kutumia huduma za bima kwa ufanisi.
“Uelewa hujenga imani, na imani huongeza matumizi endelevu ya bima,” amesema.
Amesema Tanzania inaingia katika hatua muhimu ya kujenga familia zenye uwezo wa kustahimili misukosuko ya kifedha na taifa lenye uimara wa kifedha, huku bima ya maisha ikiwa na nafasi muhimu katika kulinda wananchi na kusaidia mipango yao ya muda mrefu.
Amesema matumizi ya lugha ya Kiswahili katika bidhaa hizo ni hatua muhimu katika kuongeza uelewa na ujumuishi wa huduma za bima nchini.
“Matumizi ya lugha inayoeleweka katika kutoa taarifa na elimu kuhusu bima huwawezesha wananchi kuelewa kwa usahihi faida, masharti na wajibu wao kabla na baada ya kujiunga na bima,” amesema.
Pamoja na hayo amesema kuwa bima ya maisha ni nyenzo muhimu katika kujenga usalama wa kifedha na uwezo wa kustahimili changamoto kwa mtu binafsi, familia na taifa kwa ujumla.
Social Plugin