Na Dotto Kwilasa,DODOMA
Ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Urusi imeendelea kuzaa matunda kwa Tanzania, baada ya wanafunzi 10 waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kidato cha sita kupata ufadhili wa kusoma katika Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University), jijini Moscow.
Wanafunzi hao, waliomaliza kidato cha sita na kupata alama za juu katika tahasusi za PCM, PGM na PMC, wamepata nafasi hiyo kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended, ikiwa ni sehemu ya fursa zilizofunguka kufuatia ziara ya Rais Samia nchini Urusi mwezi Juni mwaka huu.
Ziara hiyo pia ilihusisha tukio la kihistoria ambapo RUDN University ilimtunuku Rais Samia Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa), na sasa imeendelea kutoa fursa kwa vijana wa Kitanzania kupata elimu ya juu nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 13, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema wanafunzi hao wamechaguliwa kutokana na kufanya vizuri katika matokeo yao ya kidato cha sita.
Prof. Mkenda amesema wanafunzi hao 10 ni sehemu ya kundi la wanafunzi waliofanya vizuri baada ya wanafunzi 50 wa awali, ambapo wamechaguliwa kuanzia nafasi ya 51 hadi 60.
Amesema kati ya wanafunzi hao, wanane wametoka katika shule za Serikali na wawili kutoka shule binafsi, huku wakitarajiwa kupata mafunzo ya awali nchini Urusi kwa kipindi cha takribani miezi 10.
“Wanafunzi hao wanatarajiwa kufanya kambi ya mafunzo nchini Urusi kwa takribani miezi 10. Serikali ya Urusi itagharamia mafunzo hayo kwa asilimia 80 na Serikali ya Tanzania itagharamia asilimia 20. Watakapoanza mafunzo ya chuo kikuu mnamo Septemba 2027, Serikali ya Urusi itagharamia kwa asilimia 100,” amesema Prof. Mkenda.
WANAFUNZI 50 WA AWALI KUANZA KAMBI SEPTEMBA
Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda amesema wanafunzi 50 waliochaguliwa awali kwa ajili ya ufadhili wa masomo nje ya nchi wamekubali fursa hiyo na wanatarajiwa kuanza kambi ya mafunzo Septemba 14, 2026.
Amesema kambi hiyo itafanyika katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Arusha, kwa kipindi kisichozidi miezi 10 kabla ya wanafunzi hao kuendelea na masomo katika vyuo vya nje ya nchi.
MKENDA AWATAKA WANAFUNZI KUFANYA VIZURI
Prof. Mkenda amewataka wanafunzi wanaopata ufadhili wa kusoma nje ya nchi kutumia vizuri fursa hizo kwa kufanya vizuri katika masomo yao.
Amesema mafanikio ya wanafunzi hao yataongeza imani kwa nchi zinazotoa ufadhili na kusaidia Tanzania kupata fursa zaidi za ufadhili kwa wanafunzi wengine.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hiyo pia itasaidia kuongeza fursa za elimu ya juu kwa Watanzania na kupunguza mzigo wa mikopo ya elimu ya juu, hivyo kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kupata nafasi za kusoma katika vyuo vikuu.

Social Plugin