Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UKUBWA WA DHAMANA YANGU UTAPIMWA KWA UTII KWA RAIS, UADILIFU KWA WATANZANIA - MAKAMU RAIS MTEULE NDEJEMBI


MAKAMU wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema ukubwa wa dhamana aliyopewa hautapimwa kwa umri au ujana wake, bali kwa utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uadilifu kwa Watanzania na utekelezaji wa majukumu atakayopewa.

Ndejembi amesema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyomuwekea kwa kumpa dhamana mbalimbali serikalini, ikiwemo kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Waziri wa Nishati, kabla ya kumteua kuwa Makamu wake wa Rais.

Amesema uteuzi huo ni ishara ya imani kubwa aliyooneshwa na Rais Samia, huku akiahidi kutumia nafasi hiyo kwa unyenyekevu katika kumsaidia Rais kutekeleza majukumu yake na kuwa kiungo kwa Watanzania.
“Nafahamu ukubwa wa dhamana hii hautapimwa kwa ujana wangu peke yake. Dhamana yangu itapimwa kwa utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uadilifu kwa Watanzania na kazi yoyote nitakayotumwa na mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Ndejembi.

Aidha, amekishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa imani kilichoionesha kwake baada ya jina lake kujadiliwa katika Kamati Kuu na kuungwa mkono na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuwa msaidizi wa kwanza wa Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndejembi amesema imani hiyo si kwake binafsi pekee, bali ni ishara kwamba CCM inaendelea kulea, kuwaamini na kuwaandaa vijana kushika dhamana mbalimbali za uongozi nchini.
Ameeleza kuwa amekulia ndani ya CCM na amepata nafasi za kuhudumu katika Baraza Kuu la UVCCM, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na baadaye serikalini kama Mkuu wa Wilaya, Mbunge, Naibu Waziri na Waziri, hatua iliyomfikisha katika nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


“Najua nafasi hii si ya mtu mmoja bali ni ya taifa letu na Watanzania. Nakuwa Makamu wa Rais si wa CCM pekee, bali nakwenda kuwa Makamu wa Rais wa Watanzania wote na wa vyama vyote,” amesema.


Ndejembi amesema atajitahidi kwa unyenyekevu mkubwa kumsaidia Rais Samia katika kutekeleza majukumu yake na kuhakikisha anakuwa kiungo kwa Watanzania wote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com