Wakati wapo baadhi ya watu wanaotaka nchi yao ifikiriwe vibaya, wapo pia wale wanaoiona iko vizuri na kuishukuru kwa juhudi zake kubwa za kusaidia nchi nyingine, kujimudu katika mambo mbalimbali.
Jamhuri ya Afrika Kusini ni moja ya nchi zinazoishukuru Tanzania na kuipongeza kwa mchango na juhudi zake katika kupunguza tatizo la njaa na kuimarisha usalama wa chakula katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Pongezi hizo zilitolewa na Waziri wa Uhusiano wa Kitaifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, wakati akihitimisha Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika Agosti 12 hadi 14 mwaka huu jijini Durban, Afrika Kusini, ambapo alibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuongeza uzalishaji wa chakula.
Kauli hiyo ilitolewa siku moja tu baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Millya, kueleza kuwa uzalishaji wa chakula nchini umeongezeka kutoka tani milioni 22.80 mwaka 2024/2025 hadi tani milioni 23.80 mwaka 2025/2026, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 4.3, huku kiwango cha taifa cha kujitosheleza kwa chakula kifikia asilimia 130 na hivyo kuwezesha nchi kuwa na ziada ya kusaidia nchi nyingine wanachama wa SADC.
Mbali na Tanzania, Lamola alizipongeza pia Zambia, Zimbabwe na Namibia kwa hatua walizopiga katika kupunguza njaa, huku akisisitiza kuwa licha ya mafanikio hayo, bado watu milioni 58 katika ukanda huo wanaishi katika hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula, jambo linalowataka viongozi na nchi wanachama chini ya uenyekiti wake wa SADC kwa kipindi cha Agosti 2026 hadi Agosti 2027 kuongeza kasi ya uzalishaji wa kilimo, kuimarisha biashara ya mazao, na kutekeleza mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Social Plugin