Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SIMBA SC YAANDIKA HISTORIA NGORONGORO, YAFUNGUA UKURASA MPYA WA MAADHIMISHO YA MIAKA 90

Na Mwandishi wetu, Ngorongoro.

Klabu ya Simba SC imeweka alama nyingine katika historia yake baada ya kuzindua rasmi ratiba ya matukio ya kuadhimisha miaka 90 tangu kuanzishwa kwake, huku kilele cha sherehe hizo kikitarajiwa kufanyika katika eneo la kipekee la Hifadhi ya Ngorongoro.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kuunganisha historia, utamaduni na utalii wa Tanzania sambamba na kuonyesha ukubwa wa Simba ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Akizungumza Agosti 1,2026 kuhusu ushirikiano huo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Aidan Makala, amesema ushirikiano kati ya NCAA na Simba SC utakuwa fursa muhimu ya kutangaza vivutio vya Tanzania na kuendeleza mahusiano kati ya sekta ya michezo na utalii.

Amesema Ngorongoro na Simba SC vina mambo mengi yanayofanana, ikiwemo kuwa alama zinazowakilisha nguvu na ubora. Kwa upande mmoja, Ngorongoro ni miongoni mwa maeneo maarufu ya urithi wa dunia, huku Simba ikiwa miongoni mwa klabu zenye historia kubwa na mafanikio katika soka la Afrika.

Aidha Makala ameongeza kuwa matukio makubwa kama haya yana nafasi ya kuhamasisha Watanzania kutembelea maeneo ya utalii na kuendelea kuthamini urithi wa taifa.

Kwa upande wa Simba SC, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Suleiman Harun, amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kumbukumbu ya safari ndefu ya klabu hiyo ambayo imekuwa ikijenga historia kwa miaka 90.

Amesema uchaguzi wa Hifadhi ya Ngorongoro kuwa sehemu ya tukio hilo umefanyika kwa lengo la kuonyesha utofauti wa Simba na kuunganisha mafanikio ya michezo na uzuri wa vivutio vya Tanzania.

“Simba imeendelea kuwa klabu yenye ubunifu na upekee, hivyo tunashukuru ushirikiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika kufanikisha tukio hili,” amesema Harun.

Pia , amewataka mashabiki wa Simba kuendelea kuiunga mkono timu hiyo huku akisisitiza kuwa mwaka wa maadhimisho ya miaka 90 utakuwa wa matukio mbalimbali yatakayowakutanisha Wanamsimba na wadau wa klabu hiyo.

Naye Msemaji wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema uamuzi wa kupeleka maadhimisho ya Wiki ya Simba katika Hifadhi ya Ngorongoro unatokana na dhamira ya klabu hiyo kufanya matukio yenye mvuto tofauti na yaliyowahi kufanyika hapo awali.

Amesema hatua hiyo inalenga pia kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia michezo na utalii, huku akibainisha kuwa Simba itaendelea kuweka mikakati mipya yenye kuleta thamani kwa mashabiki wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com