Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAIMARISHA UDHIBITI WA MADUKA YA DAWA MUHIMU



Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na udhibiti wa Maduka ya Dawa Muhimu (DLDM) nchini ili kuhakikisha huduma za dawa zinazotolewa kwa wananchi zinazingatia sheria, kanuni na viwango vya kitaalamu.

Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Agosti 17, 2026, jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kuhusu mchakato na taratibu za utungaji wa Kanuni za Ukaguzi wa Maduka ya Dawa Muhimu mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa.

Amesema hatua hizo ni muhimu katika kulinda afya za wananchi kwa kuhakikisha dawa zinahifadhiwa na kutolewa kwa usahihi, huku watoa huduma wakiwa na sifa na leseni zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Dkt. Samizi amesema Serikali pia inaendelea kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa maduka hayo, ikiwemo baadhi ya wamiliki kuajiri watu wasio na sifa za kutoa huduma za dawa, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa wananchi.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikisha wadau katika maboresho ya kanuni za usimamizi wa DLDM ili kuhakikisha taratibu zinazowekwa zinaendana na mahitaji ya huduma za afya na kulinda maslahi ya wananchi.

Kwa upande wake, taarifa hiyo imeeleza kuwa mchakato wa maboresho ya Kanuni za DLDM za mwaka 2019 unaendelea, huku wadau mbalimbali, wakiwemo wamiliki wa maduka hayo, wakitarajiwa kushirikishwa katika mchakato huo.

Dkt. Samizi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa huduma za dawa kwa kuzingatia sheria na kanuni, ili kuzuia matumizi holela ya dawa, uwepo wa dawa zisizo salama na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com