Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RIJK ZWAAN YAWAJENGEA WAKULIMA UWEZO WA KULIMA KWA TIJA NA SOKO LA UHAKIKA


Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Harufu ya ubunifu wa kilimo, mbegu bora na teknolojia za kisasa imeanza kutawala viwanja vya Maonesho ya Wakulima Nanenane jijini Dodoma, huku kampuni ya Rijk Zwaan Tanzania,ikitumia jukwaa hilo kuwawezesha wakulima kupata maarifa yatakayowaongezea tija na kipato.

Rijk Zwaan Tanzania, ni miongoni mwa kampuni zinazovutia umati wa wakulima ambayo imekuja na mbegu bora za mazao ya mboga mboga pamoja na elimu ya uzalishaji wenye tija na uhakika wa soko.

Akizungumza leo Agosti 3,2026 katika maonesho hayo, Mtaalamu Mwandamizi wa Maendeleo ya Bidhaa na Afisa wa Kilimo wa Rijk Zwaan Tanzania, Neiman Mollel, amesema kampuni hiyo imejipanga kuwafikia wakulima wengi zaidi kupitia maonesho ya Nanenane kwa kuwapa elimu ya kina kuhusu uzalishaji wa mboga mboga zenye ubora wa kimataifa.

Amesema kampuni hiyo kwa sasa inafanya kazi katika mikoa minne ambayo ni Dodoma, Arusha, Morogoro na Mwanza, ambako imeendelea kuwasaidia wakulima kupata mbegu bora pamoja na ushauri wa kitaalamu unaowezesha kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko.

Mollel amesema wakulima wanaotembelea banda la kampuni hiyo wanapata nafasi ya kujifunza namna bora ya kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo pilipili hoho, nyanya, kabichi, karoti na mboga nyingine zinazohitajika sana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa mbali na kuuza mbegu, kampuni hiyo imeweka mkazo katika kuwajengea wakulima uwezo wa kuelewa mahitaji ya soko kabla ya kuanza uzalishaji, hatua ambayo husaidia kupunguza hasara na kuongeza faida kwa mkulima.


Kwa upande wake, Mhamasishaji wa kampuni hiyo, Ray Peter Mark, amewakaribisha wakulima, vijana na wananchi wote kutembelea banda la Rijk Zwaan katika Maonesho ya Nanenane ili kujifunza teknolojia mpya za kilimo cha mboga mboga na kupata ushauri wa wataalamu.

Amesema vijana wengi wanaotembelea banda hilo huonesha hamasa ya kuingia kwenye kilimo lakini changamoto kubwa wanayoieleza ni ukosefu wa mitaji ya kuanzisha shughuli hizo.

Hata hivyo, amesema changamoto hiyo inaweza kutatuliwa kwa kutumia fursa zilizowekwa na Serikali.

"Serikali imeweka mifuko mbalimbali ya kuwawezesha vijana kupitia Wizara ya Vijana pamoja na asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri zinazotolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu,

Nawahimiza vijana kujiunga kwenye vikundi ili waweze kunufaika na fedha hizo na kuanzisha kilimo cha kisasa," amesema.

Mark ameongeza kuwa kampuni hiyo inaendelea kuwashauri wakulima kuchagua mbegu bora zinazokidhi mazingira yao, kupanga uzalishaji kulingana na mahitaji ya soko na kutumia teknolojia sahihi za kilimo ili kuongeza tija, huku Rijk Zwaan ikiendelea kuwaunganisha na masoko yanayohitaji mazao yenye ubora wa hali ya juu.














Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com