Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA : TUITUNZE AMANI KWANI NDIO MSINGI WA MAENDELEO

Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa wananchi kulinda amani kama msingi mkuu wa maendeleo na kuenzi dhana ya mapinduzi ili iwe chachu ya kuleta mabadiliko bora ya kiuchumi na kijamii. 

Alisema wananchi wanapaswa kuendelea kuitunza amani na kuenzi dhana ya mapinduzi kwa kuhakikisha inakuwa chachu ya maendeleo.

“Tunaposema Mapinduzi daima, Mapinduzi ya juzi ni ya maendeleo. Tunapindua yaliyokuwepo ambayo tulikuwa nyuma, tunaleta maendeleo bora zaidi. Hiyo ndiyo maana ya Mapinduzi,” alisema Rais Samia.

Alihimiza wananchi wawe walinzi wa miundombinu, ikiwemo ya mradi wa maji kwa kuwa zimetumika fedha nyingi na utaalamu.

“Miradi hii ni uhai wetu, ni fursa zetu, ni uchumi wetu na ustawi wa maisha yetu… Ni wajibu wetu na ni lazima ndugu zangu tuitunze miradi hii kama tunavyotunza macho yetu,” alisema Rais Samia.

Akizungumza na wananchi baada ya kuzindua mradi wa maji wa Kizimkazi wakati wa Tamasha la Kizimkazi, Rais Samia alisema amani imewezesha kupata maendeleo, hivyo wananchi wailinde kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha ameagiza Wizara ya Maji Zanzibar na Wizara ya Maji ya Serikali ya Muungano zishirikiane kuhakikisha mpango wa kujenga gridi ya maji Wilaya ya Kusini unatekelezwa.

Alisema ameelezwa mpango huo unahusisha ujenzi wa matangi katika maeneo tofauti ya wilaya ili kuimarisha upatikanaji wa maji.

“Shirikianeni kuhakikisha hilo linatokea, kwamba gridi ya wilaya inajengwa na hilo linatokea,” alisema Rais Samia.

amewapa maagizo manne huku akiwataka wananchi kuwa walinzi thabiti wa miundombinu hiyo ya maji na kuitunza kama wanavyotunza macho yao kutokana na fedha na utaalamu mkubwa uliotumika. 

Pia, Rais Samia ameagiza maji katika mradi wa Kizimkazi yasambazwe hadi Kibuteni na Mtende na kama Makunduchi kuna upungufu wa maji, yafikishwe na huko.

Alisema uwezo wa mradi mpya wa Kizimkazi umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye, ukiwa takribani mara mbili ya mahitaji ya sasa.

Vilevile, Rais Samia alieleza kuridhishwa na maendeleo ya Kituo cha Afya Kizimkazi, akisema kinaendelea kukua na kutoa huduma zinazokaribia kiwango cha hospitali ya wilaya.

Alisema kituo hicho kinatoa huduma za matibabu ya kusafisha figo na huduma nyingine zikiendelea kuboreshwa, ukiwemo mpango wa kuanzisha tiba ya mazoezi.

Rais Samia alisema uwanja wa michezo unaojengwa Kizimkazi unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu au Januari mwakani na kwamba maandalizi ya huduma za afya yanapaswa kwenda sambamba na uwanja huo.

Alisema jana asubuhi alitembelea Kituo cha Afya Kizimkazi ambako Shirika la Afya Duniani (WHO) lilimkabidhi gari la wagonjwa lenye vifaa kwa ajili ya kituo hicho.

Aidha, Rais Samia alisema alipanda mti jana na kukagua huduma za afya na maendeleo ya huduma za wagonjwa wa figo.

Pia, alitembelea eneo la ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kizimkazi kinachojengwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Taasisi ya Samia na mkandarasi QBS.

Rais Samia alisema Kizimkazi imekuwa ikikabiliwa na tatizo la maji kwa muda mrefu.

Alisema tangi la awali la Kizimkazi lilijengwa mwaka 1994 likiwa na uwezo wa lita 150,000 lakini baadaye lilishindwa kukidhi mahitaji kutokana na ongezeko la watu, uwekezaji na changamoto za kitaalamu na uharibifu uliotokana na mazingira.

Rais Samia alisema serikali iliamua kuwekeza katika mradi mpya wenye uwezo mkubwa zaidi ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com