Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Benki ya NMB imeendelea kuimarisha uhusiano wake wa kimkakati na Bunge la Tanzania kwa kudhamini Bonanza la Michezo la Bunge la 13, hatua inayolenga kuimarisha afya, mshikamano na mahusiano ya kikazi miongoni mwa watumishi wa Bunge pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali.
Bonanza hilo linatarajiwa kufanyika kesho Agost 29,2026 kuanzia saa 12:00 asubuhi kuanzia Viwanja vya Chuo Cha Mipango kuelekea Viwanja vya John Merin Secondary School, Dodoma, likiwa sehemu ya juhudi za Bunge kutumia michezo kama nyenzo ya kuimarisha afya na kujenga ushirikiano na wadau wake.
Katika bonanza hilo, Wizara 14 na Taasisi 10 zimealikwa kushiriki, huku washiriki wakipata fursa ya kushindana na kujenga mahusiano kupitia michezo mbalimbali ikiwamo mpira wa wavu, pete, kikapu, kuvuta kamba na mbio.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya bonanza hilo Mwenyekiti wa Bunge bonanza Festo Sanga amesema michezo ni sehemu muhimu ya maisha ya watumishi kwa kuwa husaidia kuimarisha afya ya mwili, akili na mahusiano ya kijamii.
Amesema Bunge limeamua kuendeleza na kupanua wigo wa ushirikiano na wadau wake, likitambua kuwa ushirikiano huo unaweza kwenda zaidi ya shughuli za kawaida za kibunge na kugusa maeneo muhimu ya kijamii, ikiwamo afya na ustawi wa wananchi.
“Michezo ni afya. Mazoezi yanasaidia kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza na wakati huo huo yanatuleta pamoja,” amesema.
Kwa mtazamo huo, amesema bonanza hilo linatoa nafasi kwa Bunge, Serikali na taasisi washirika kukutana katika mazingira yasiyo rasmi, kujenga urafiki, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano.
Bonanza hilo ni miongoni mwa matukio makubwa ya kimichezo yanayofanyika katika Bunge la 13, huku Mhe. Zungu akiwa mgeni rasmi.
NMB: TUNARUDISHA THAMANI KWA JAMII
Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo Cha mahusiano ya benki na Serikali Vicky bishubo amesema ushirikiano wa benki hiyo na Bunge una historia iliyojengwa katika msingi wa kuwa na mahusiano ya kimkakati yanayolenga kuleta thamani kwa pande zote pamoja na jamii kwa ujumla.
Amesema benki hiyo inatambua nafasi ya Bunge kama taasisi muhimu katika maendeleo ya Taifa na kwamba imekuwa ikithamini fursa mbalimbali za kushirikiana nalo.
Amesema NMB itaendelea kuboresha huduma zake na kushirikiana na taasisi za Serikali na jamii katika maeneo ambayo yanaweza kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
“Mahusiano yetu na Bunge ni ya kihistoria na kama mashirika ya kimkakati tunayathamini. Tunaahidi kuendelea kuboresha huduma zetu kwa jamii na wakati wowote tunahitaji muendelee kutushirikisha,” amesema.
Ameongeza kuwa udhamini wa bonanza hilo ni sehemu ya dhamira ya NMB ya kurudisha thamani kwa jamii, huku michezo ikiwa moja ya maeneo yanayoweza kuunganisha watu, kuhamasisha maisha yenye afya na kujenga mahusiano.
Licha ya hayo amesema NMB imewezesha upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya michezo vitakavyotumika katika bonanza hilo, ikiwamo mipira na vikombe vya ushindi, pamoja na mahitaji mengine yanayohitajika ili kuhakikisha tukio linafanyika katika mazingira bora.
UDHAMINI WA NMB NA THAMANI KWA JAMII
Udhamini huo unaipa NMB nafasi ya kuonekana siyo tu kama taasisi inayotoa huduma za kifedha, bali pia kama mshirika anayeshiriki katika shughuli za kijamii na ustawi wa jamii.
Kwa upande wa biashara, ushirikiano wa aina hiyo unajenga uhusiano wa muda mrefu kati ya taasisi za fedha na taasisi za umma, huku ukiipa sekta binafsi fursa ya kutumia nguvu zake kusaidia shughuli zinazogusa moja kwa moja maisha ya watu.
Kwa Bunge, ushirikiano huo unawezesha kupata mazingira bora ya kuendesha bonanza bila kubeba gharama zote za maandalizi, huku NMB ikipata fursa ya kuonyesha kwa vitendo dhamira yake ya kushiriki katika maendeleo ya jamii.
NMB imeendelea kusisitiza kuwa dhamira yake ni kuweka jamii katika kiini cha shughuli zake, na udhamini wa bonanza hilo ni sehemu ya utekelezaji wa dhana hiyo kupitia michezo, afya na mahusiano ya kijamii.
BURUDANI NA MSHIKAMANO
Mbali na ushindani wa michezo, bonanza hilo linatarajiwa kuwa na mazingira ya burudani na ushirikiano, likiwaleta pamoja wabunge, watumishi wa Bunge, viongozi, watumishi kutoka wizara na taasisi mbalimbali pamoja na wadau wengine.
Washiriki watapata nafasi ya kushiriki katika michezo kwa lengo la kushindana, kujenga afya na kuimarisha mahusiano, huku uwepo wa zawadi na vikombe ukiongeza hamasa ya ushindani.
Kwa Bunge, tukio hilo linawakilisha hatua nyingine katika kutumia michezo kama sehemu ya kujenga taasisi yenye watumishi wenye afya, mshikamano na ari ya kutekeleza majukumu yao.
Aidha, ushiriki wa wizara 14 na taasisi 10 unaifanya bonanza hiyo kuwa zaidi ya mashindano ya ndani ya Bunge, kwani inafungua fursa ya kuimarisha mtandao wa mahusiano kati ya Bunge na taasisi mbalimbali za Serikali.
Kwa wananchi, tukio hilo pia linatoa fursa ya kuona namna taasisi za umma na sekta binafsi zinavyoweza kushirikiana katika maeneo ya kijamii huku zikiendelea kutekeleza majukumu yao ya msingi.
Michezo, afya na ushirikiano ndivyo vinavyobeba ujumbe wa Bonanza la Michezo la Bunge la 13, huku NMB ikiwa mshirika mkuu katika kufanikisha tukio hilo.




Social Plugin