Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKENDA KUFUNGUA JUKWAA LA UBUNIFU TANGA

 



Na Oscar Assenga, Tanga

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026, inayofanyika katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga.

Maonyesho hayo yaliyoanza Agosti 15 na yanatarajiwa kuendelea hadi Agosti 24, mwaka huu, yanalenga kuonyesha mchango wa elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa kupitia Dira ya Taifa 2050.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya maonyesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian, alisema mkoa huo umejiandaa kikamilifu kumpokea Profesa Mkenda pamoja na washiriki wengine watakaohudhuria tukio hilo.

Dk Batilda alisema Serikali ya Mkoa imeimarisha maandalizi, ikiwemo ulinzi na usalama, ili kuhakikisha washiriki na wananchi wanaotembelea maonyesho hayo wanapata mazingira salama na rafiki.

“Tanga inajivunia kuwa mwenyeji wa maonyesho haya. Tunawahakikishia Wizara ya Elimu na wananchi kuwa Serikali ya Mkoa imejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa wakati wote wa maonyesho,” alisema.

Alisema maonyesho hayo ni fursa muhimu kwa wananchi kujionea kwa vitendo namna Serikali, taasisi za elimu, watafiti na wabunifu wanavyoshiriki katika kuleta maendeleo ya Taifa.

Kaulimbiu ya maonyesho hayo ni “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa 2050,” ambayo, kwa mujibu wa Dk Batilda, inaendana na hatua ambayo Taifa limefikia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.

Alisema kila sekta, taasisi, wizara, mkoa na halmashauri ina wajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu Dira ya Taifa 2050 na nafasi yao katika kuifikia.

“Maonyesho haya yataonyesha Tanzania tunayotaka kuifikia ifikapo mwaka 2050. Taasisi za elimu, vyuo vya ufundi, taasisi za utafiti na shule zitaonyesha mchango wao katika kufikia dira hiyo,” alisema.
Washiriki zaidi ya 300

Dk Batilda alisema zaidi ya washiriki 300 kutoka maeneo mbalimbali wanashiriki katika maonyesho hayo, wakiwemo wawakilishi kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti na maendeleo, vyuo vya mafunzo na ufundi stadi pamoja na taasisi binafsi zinazohusiana na sayansi na teknolojia.

Alisema washiriki hao watapata fursa ya kuonyesha bunifu, teknolojia, ujuzi na shughuli mbalimbali zinazohusiana na elimu na maendeleo ya Taifa.

Aidha, alisema maonyesho hayo yanatoa fursa muhimu kwa vijana wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu kupata taarifa sahihi kuhusu fursa za elimu na namna ya kufanya maombi ya kujiunga na vyuo.

“Vijana wanaoanza mchakato wa kujiunga na vyuo vikuu Mtapata fursa ya kuelekezwa namna sahihi ya kujaza maombi na kupata taarifa nyingine muhimu kuhusu elimu ya juu,” alisema.
Sh156 bilioni elimu Tanga

Katika hatua nyingine, Dk Batilda alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya elimu, akisema Mkoa wa Tanga umepokea zaidi ya Sh156 bilioni kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia.

Alisema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya elimu na kuongeza ubora wa huduma za elimu nchini.

Pia alimpongeza Profesa Mkenda na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kuunga mkono maonyesho hayo, akisema tukio hilo limeendelea kukua na kuboreshwa.

Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wananchi wa Tanga na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Usagara kushuhudia maonyesho hayo na kupata elimu kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya elimu, ujuzi, sayansi na ubunifu.

Alisema maonyesho hayo pia yatawapa wananchi nafasi ya kujionea hatua ambazo Tanzania imepiga katika matumizi ya teknolojia, utafiti na ubunifu katika kutatua changamoto mbalimbali za jamii.

Uzinduzi rasmi wa maonyesho hayo unatarajiwa kufanyika Agosti 18, 2026, ukiongozwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, huku Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga maonyesho hayo Agosti 24.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com