Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAAFISA BIASHARA WAFUNZWA NAMNA YA KUDHIBITI BIDHAA BANDIA




Na Mwandishi Wetu

Tume ya Ushindani (FCC) imetoa elimu kwa Maafisa Biashara kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya ushindani katika biashara, udhibiti wa bidhaa bandia pamoja na umuhimu wa kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa na huduma zisizokidhi viwango.

Semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo Maafisa Biashara ambao wana nafasi muhimu katika kusimamia shughuli za biashara katika maeneo yao, ili waweze kutambua changamoto zinazohusiana na ushindani usio wa haki, bidhaa bandia na vitendo vinavyoweza kuwaathiri walaji.

Akitoa mada kuhusu udhibiti wa bidhaa bandia, wakati wa Mkutano wa Maafisa Biashara nchini katika Kikao cha Tatu cha Wizara ya Viwanda na Biashara na Maafisa Biashara, kilichofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti wa Bidhaa Bandia wa FCC, Bw. Salvatory Chuwa, ameeleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya FCC na Maafisa Biashara katika kukabiliana na biashara ya bidhaa bandia.

"Bidhaa bandia zina madhara makubwa kwa uchumi, wafanyabiashara wanaofuata sheria na walaji, hivyo ni muhimu kwa Maafisa Biashara kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kubaini na kutoa taarifa kuhusu bidhaa zinazodhaniwa kuwa bandia."amesema Bw.Chuwa

Amesisitiza kuwa udhibiti wa bidhaa bandia unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, wafanyabiashara na wananchi, huku akiwataka Maafisa Biashara kutumia nafasi zao kuelimisha wafanyabiashara na walaji kuhusu madhara ya bidhaa bandia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tafiti, Miungano ya Makampuni na Uraghibishi wa FCC, Bi. Zaytun Kikula, ametoa mada kuhusu masuala ya ushindani, akieleza umuhimu wa kuwepo kwa mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki kwa ajili ya kukuza uchumi na kuwapa wafanyabiashara fursa sawa katika soko.

Bi.Kikula amebainisha kuwa ushindani wenye tija husaidia kuongeza ubunifu, kuboresha ubora wa bidhaa na huduma pamoja na kuwapa walaji fursa ya kupata bidhaa bora kwa bei shindani.

Aidha, amewataka Maafisa Biashara kushirikiana na FCC katika kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu sheria za ushindani na kuhakikisha kuwa vitendo vinavyoweza kuzuia au kupotosha ushindani vinatambuliwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Semina hiyo ni sehemu ya jitihada za FCC za kuimarisha uelewa wa wadau kuhusu wajibu wa kulinda ushindani katika soko, kudhibiti bidhaa bandia na kuhakikisha haki za walaji zinalindwa.

FCC imeendelea kusisitiza kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, hususan Maafisa Biashara, ni muhimu katika kujenga soko lenye ushindani wa haki, bidhaa salama na mazingira bora ya biashara kwa manufaa ya wafanyabiashara, walaji na uchumi kwa ujumla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com