Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

eGA YASUKUMA MAGEUZI YA KILIMO KWA MIFUMO YA KIDIJITALI



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Wakati Serikali ikiendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia katika kuongeza tija ya uzalishaji, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imeeleza kuwa mifumo ya kidijitali iliyoibuni imekuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuboresha usimamizi wa shughuli za kilimo nchini.

Akizungumza leo Agosti 2, 2026, katika Maonesho ya 88 ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Subira Kaswaga, amesema mamlaka hiyo inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali kuhakikisha huduma zote muhimu zinahamia katika mifumo ya kidijitali kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi.

Amesema kupitia ushirikiano na Wizara ya Kilimo, e-GA imeunda mfumo wa e-Kilimo unaowezesha ukusanyaji wa taarifa za wakulima, usimamizi wa taasisi zilizo chini ya wizara pamoja na utoaji wa vibali mbalimbali vinavyohusu shughuli za kilimo.

Kaswaga amesema e-GA pia imeungana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kutengeneza mfumo wa kidijitali unaorahisisha usimamizi wa vyama vya ushirika, ambapo wakulima wanaweza kufuatilia masoko ya mazao yao, mwenendo wa mauzo na kupata taarifa zinazoongeza uwazi katika shughuli za ushirika.

Aidha, amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), e-GA imeanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Mbolea (Fertilizer Information System – FIS) unaowezesha usajili wa wazalishaji na waagizaji wa mbolea, pamoja na kufuatilia bei elekezi ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa urahisi na kwa gharama stahiki.

Ameongeza kuwa e-GA imeendelea kuunganisha mifumo ya taasisi mbalimbali za Serikali, hatua inayorahisisha ubadilishanaji wa taarifa, kuondoa urasimu na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi katika sekta mbalimbali.

Kaswaga amewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nane Nane kutembelea banda la e-GA ili kujionea mifumo mbalimbali ya kidijitali inayotumiwa serikalini na kufahamu namna teknolojia hiyo inavyochangia maendeleo ya kilimo na sekta nyingine za uchumi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com