Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. SAJAD HABIB RAI AMPONGEZA MAKAMU WA RAIS NDEJEMBI, ASEMA ATAKUWA MSAADA MKUBWA KWA RAIS SAMIA


Mtaalamu katika Sekta ya Mafuta nchini, Dkt. Sajad Habib Rai, amempongeza Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa kuapishwa kushika nafasi hiyo, huku akimtabiria mambo makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, siku moja baada ya uapisho wa Makamu wa Rais huyo uliofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Dkt. Sajad amesema ana imani kubwa na kiongozi huyo, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wa Ndejembi.

Dkt. Sajad, ambaye ni Meneja Mkazi wa Mansoor Industries nchini, amesema hana shaka na uwezo wa Ndejembi katika uongozi, akisisitiza kuwa sifa na uwezo alionao ni nyenzo muhimu katika kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa kipindi kifupi alichohudumu katika Wizara ya Nishati kwa nafasi ya uwaziri, Mheshimiwa Ndejembi amekuwa mtu muhimu aliyesimama kikamilifu katika kushughulikia masuala mbalimbali. Hii ni sifa ambayo si kila kiongozi anayo,” amesema Dkt. Sajad.

Amesema hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Ndejembi na baadaye jina lake kupitishwa na Bunge inatokana na uwezo wake, jambo ambalo limemfanya kiongozi huyo Mkuu wa Nchi kujenga imani kwake. 

Hivyo, amesema Ndejembi anapaswa kuendelea kuonesha uwezo huo wakati huu anapomsaidia Rais katika majukumu makubwa zaidi ya kitaifa.

Mtaalamu huyo wa Nishati na Mawasiliano, ambaye amewahi kusaidia Serikali katika udhibiti wa mafuta bandarini kupitia ubunifu wa mfumo maalumu wa udhibiti wa mafuta (BIL), amewataka wananchi kumuamini Ndejembi na kumpa ushirikiano wakati akitekeleza wajibu wake.

Pamoja na wananchi, Dkt. Sajad amewataka pia watendaji wote wa Serikali, Wabunge pamoja na wafanyabiashara nchini, wakiwemo wale wanaofanya shughuli zao katika Sekta ya Mafuta, kuendelea kumuunga mkono Makamu wa Rais Ndejembi ili aweze kutimiza kikamilifu majukumu yake ya kumsaidia Rais Samia na kulitumikia Taifa kwa ujumla.

Ndejembi, ambaye amehudumu katika nafasi mbalimbali za utumishi na uongozi, ikiwemo kuwa Waziri wa Utumishi na baadaye Waziri wa Nishati, ameapishwa kushika nafasi ya Makamu wa Rais baada ya mtangulizi wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kujiuzulu hivi karibuni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com