Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameeleza kuwa nchi ina utoshelevu wa chakula kwa asilimia 130 na imeongeza mauzo nje ya nchi kwa asilimia 77, huku akitoa wito kwa wazalishiaji mbalimbali nchini kuboresha bidhaa zao ili zimudu ushindani wa kimataifa na ziweze kushindana kila siku na siyo wakati wa maonesho pekee.Akizungumza, Agosti Mosi, 2026 wakati akifungua Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Wakulima (Nanenane) katika Viwanja vya Dkt. John John S. Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema kuwa mafanikio hayo ya chakula na ongezeko la mauzo ya nje yanachangiwa na hatua za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi, uwekezaji wenye tija kwenye mnyororo mzima wa sekta ya kilimo, na kutoa ruzuku ya pembejeo zikiwemo zaidi ya tani 700,000 za mbolea yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.4.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa bidhaa zinazozalishwa zinapaswa kuwa na viwango vya juu vya kila siku ili zipate masoko popote duniani, akibainisha kuwa katika maeneo mengi tatizo siyo soko bali ni viwango vinavyoweza kumfanya mnunuzi atamani kununua, jambo litakaloongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho na kupata maelezo kutoka kwa wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo ambapo aliipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kuboresha huduma za kifedha na kuzisogeza karibu na wananchi hasa wakazi wa vijijini, vijana na wanawake.
Amesema amefurahishwa na jitihada za benki hiyo za kuwafikia wananchi kupitia huduma za kibenki zinazotolewa kwa kutumia magari maalumu pamoja na kuwafuata wafanyabiashara katika masoko na minada mbalimbali nchini.
“Hatua hizi zinaendana na kiu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuona Watanzania wengi wanapata huduma za uchumi jumuishi wa kifedha (financial inclusion) na hii itasaidia nchi kuondoka kwenye cash economy, itafanya tufike mahali mtu popote alipo ana fedha yake, na hata akitaka mahitaji fedha anayo,” amesema.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya sekta ya fedha, ikiwemo kupunguza gharama za miamala ya kifedha ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma bora za kibenki na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya uchumi.


Social Plugin