Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Baada ya Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba kutembelea Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane 2026 leo Agosti 1 jijini Dodoma, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeanza kutoa huduma zake moja kwa moja kwa wafanyabiashara, wakulima na wananchi, ukiwalenga kuwafikishia huduma za usajili, utoaji wa leseni pamoja na elimu ya urasimishaji wa biashara.
BRELA imesema huduma hizo zitatolewa katika viwanja vya maonesho kuanzia leo Agosti 1 hadi Agosti 8, 2026, ili kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali kwa urahisi bila kulazimika kufika katika ofisi za taasisi hiyo.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Usajili wa BRELA, Yusuf Mwasakafika, amesema wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, utoaji wa leseni za biashara Kundi A pamoja na huduma zinazohusiana na usajili wa alama za biashara na viwanda.
Amesema uwepo wa BRELA katika maonesho hayo unalenga pia kuwahamasisha wakulima wanaofanya kilimo cha kibiashara kurasimisha shughuli zao ili waweze kufanya biashara kwa kujiamini zaidi na kunufaika na fursa za masoko.
"Tunawahamasisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanaofanya shughuli mbalimbali za kilimo kufika hapa na kupata huduma ambazo wangeweza kuzitafuta wakiwa ofisini, lakini sasa wanaweza kuzipata hapa," amesema Mwasakafika.
Aidha, amesema BRELA inatumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu mfumo mpya wa usajili ulioboreshwa, ambao umelenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya wafanyabiashara.
Kwa mujibu wa Mwasakafika, kupitia mfumo huo mpya baadhi ya huduma sasa zinaweza kufanyika kwa njia ya mtandao bila mhusika kulazimika kufika moja kwa moja katika ofisi za BRELA.
Amesema miongoni mwa maboresho yaliyofanyika ni kuwezesha uwasilishaji wa nyaraka mbalimbali kwa njia ya mfumo, ikiwemo nyaraka zinazohusiana na madeni yanayohitaji kuwasilishwa katika usajili.
"Kwa kutumia mfumo huu sasa tumeweza kuboresha huduma kiasi kwamba mtu anaweza kuwasilisha nyaraka akiwa nyumbani kwake au benki, bila kulazimika kufika BRELA," amesema.
Mwasakafika amesema mfumo huo pia umeimarisha upatikanaji wa taarifa za kampuni na usalama wa taarifa za wanahisa, huku ukiwapa taarifa kila kampuni inapofanya mabadiliko muhimu yanayowahusu.
Amewataka wananchi wanaotaka kutumia mfumo huo kuhakikisha wanakuwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), namba ya simu inayotumika pamoja na anuani sahihi ya barua pepe ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Katika Maonesho ya Nane Nane, BRELA inapatikana katika banda la Makamu wa Rais na Waziri Mkuu pamoja na banda la Wizara ya Viwanda na Biashara kwa lengo la kusogeza huduma na elimu ya urasimishaji wa biashara karibu na wananchi.

Social Plugin