Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KABUDI AKAGUA NA KUKABIDHI MIRADI YA IFAD YA KUIMARISHA UZALISHAJI WA MBEGU NZEGA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, leo Agosti 17, 2026, ametembelea, kukagua na kukabidhi miradi inayotekelezwa kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi katika Shamba la Mbegu la Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA), Kilimi, Wilaya ya Nzega, Mkoa wa Tabora. 

Programu hiyo inafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo, ikiwa na lengo la kuongeza tija, kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Kabudi amesema sekta ya kilimo ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake katika pato la Taifa, usalama wa chakula, ajira na biashara ya nje. 
Amesisitiza kuwa programu hiyo ni muhimu sana kwa kuwa inalenga kuongeza tija katika sekta inayochangia kiasi kikubwa cha ajira, chakula na bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Aidha, Waziri Kabudi amekabidhi rasmi jengo la ofisi, jengo la karakana na jengo la kukaushia mbegu kwa Wizara ya Kilimo, miradi ambayo imetekelezwa kupitia programu hiyo kwa ufadhili wa IFAD. Kabla ya kukabidhi, alikagua miundombinu mbalimbali ikiwemo eneo la kukaushia mazao, ukumbi wa mafunzo na nyumba za watumishi, huku mpango huo pia ukiwa umewezesha upatikanaji wa zana za kisasa za kilimo kama vile matrekta, matillisho, na magari ya usambazaji wa mbegu.

Akihitimisha ziara hiyo, Prof. Kabudi amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa miradi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango na ubora uliokusudiwa ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha iliyowekezwa inapatikana, sambamba na kuwa na mpango mkakati madhubuti wa kufikia malengo. 

Katika ziara hiyo, Waziri Kabudi ameambatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mhandisi Athumani Kilundumya, Mkurugenzi wa Sera na Uratibu, Bw. Paul Sangawe, na Mratibu wa Programu hiyo, Bw. Salimu Mwinjaka

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com