Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAVUNDE AZINDUA HELIKOPTA YA KISASA YA BARRICK KWA AJILI YA UTAFITI WA KIJIOLOJIA MKOANI MARA

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akiwa ndani ya helikopta ya kisasa ya Barrick iliyozinduliwa kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia mkoani Mara.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akikata utepe kuzindua rasmi helikopta ya kisasa ya Barrick kwa ajili ya utafiti wa kijiolojia mkoani Mara. Wengine pichani ni viongozi wa Mkoa wa Mara pamoja na viongozi wa Barrick nchini.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara,Apolinary Lyambiko akitoa maelezo kwa Waziri Mavunde kuhusu shughuli za utafiti zitakazofanywa na helikopta hiyo mkoani Mara.
Muonekano wa helikopta ya kisasa ya Barrick iliyozinduliwa kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia mkoani Mara.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa helikopta ya kisasa ya Barrick kwa ajili ya utafiti wa kijiolojia mkoani Mara.
                                                  **
👉Kutumika pia kusaidia tafiti maeneo ya wachimbaji wadogo Tarime

Waziri wa madini, Mhe. Anthony Mavunde amezindua helikopta ya kisasa ya kampuni ya Barrick wilayani Tarime mkoani Mara kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia wa anga wenye kupunguza athari za kimazingira na kuboresha shughuli za utafutaji wa madini kufanikisha utekelezaji wa program ya Kesho Iliyo Bora Zaidi kwa sekta ya madini (Mining for Brighter Tomorrow )inayolenga kuwezesha Vijana,Wanawake na watu wenye mahitaji maalum.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa helikopta hiyo sambamba na Programu hiyo uliofanyik katika viwanja vya sekondari ya Ingwe Nyamongo wilayani Tarime , Waziri Mavunde amesema kuwa mahusiano kati ya Mgodi wa Barrick North Mara na wachimbaji wadogo na wananchi wa mji wa Nyamongo , Wilaya ya Tarime vijjijini unazidi kuimarika kwa pande zote kuanza kufanya kazi kwa pamoja.

Aliongeza kwamba mpango wa kampuni ya Barrick kuongeza nyenzo za kufanya utafiti wa kijiolojia kwenye eneo lao la kilomita za mraba 6,000 na kwa mita 30 kutoka ardhini kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu ya kisasa zaidi (high-resolution airborne geophysical surveys) ambayo huongeza usahihi wa upatikanaji wa taarifa za miamba iliyo chini ya ardhi, kupunguza athari za kimazingira na kuboresha ufanisi wa shughuli hizo.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa helikopta ya kisasa ya Barrick kwa ajili ya utafiti wa kijiolojia mkoani Mara.

“Baada ya mashauriano na uongozi wa Barrick kuhusu namna ya kufanya kazi na wananchi wa maeneo haya, Barrick walikubali kukurudisha leseni ya baadhi ya maeneo ambayo ilifanya tafiti zikagawiwa kwa vijana wa Nyamongo kwa ajili ya uchimbaji,”

“Lakini leo hii tunaanza safari ya mafanikio makubwa na vijana wa Nyamongo wanaanza uchimbaji wa madini kwa uhakika zaidi baada ya kampuni ya Barrick kukubali kutoa helikopta yake kwa ajili ya utafiti wa kitalaamu kwenye maeneo yao, haya ni mafanikio makubwa kwa vijana , wakinamama na watu wenye makundi maalum,” alisisitiza Waziri Mavunde.

Aliongeza kuwa serikali kupitia Taasisi za Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambayo ina umri wa miaka 101 imefanya kazi ya kupima ya ramani ya madini kwa 97% na utafiti wa kina na mipasuko wa miamba kwa asilimia 16% tu.

“Kutokana na taarifa hizi serikali ya awamu ya sita kupitia Dkt Samia Suluhu Hassa alitoa maeleleko ya kutenga asilimia 10% ya mapato yanayotokana kwenye sekta ya madini ili kufanya utafiti wa kina nchini nzima”,alisema.

Alisisitiza kuwa sekta ya madini inahitaji uwekezaji kwenye teknolojia na sayanasi ili kuweza kufanya utafiti kisasa zaidi kwa kutumia helikopta ili kuleta kasi ya matokeo chanya pamoja na kuendelea kulinda mazingira.

Pamoja na mambo mengine , Waziri Mavunde akizungumza kuhusu programu ya kesho iliyopo bora kwa sekta ya madini (Mining for Brighter Tomorrow) alisisitiza kwamba ni shauku ya Serikali na Wizara ya Madini kuona kwamba wanawake , vijana na watu wenye ulemavu kuingia na kushiriki zaidi kwenye sekta ya madini nchini.

Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Barrick nchini , Dkt. Melkiory Ngido, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha sekta ya madini nchini na kufungua milango ya tafiti kwa kutumia nyenzo za kisasa na kuwashirikisha wachimbaji wadogo ili kupanua mnyororo wa thamani.
Meneja Mkazi wa Barrick nchini Tanzania, Dkt. Melkiory Ngido, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa helikopta ya kisasa ya kampuni hiyo kwa ajili ya utafiti wa kijiolojia mkoani Mara.

Dkt. Ngido aliongeza kuwa uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ni muhimu katika utekelezaji wa sera ya madini ya Taifa, inayolenga kuimarisha utafiti wa rasilimali madini, kuongeza thamani ya sekta ya madini katika uchumi wa taifa na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa ufanisi zaidi huku uchangiaji kwenye maendeleo ya nchini ukiendelea kukua kwa kasi.

“Napenda kuchukua fursa kukushuru Waziri wa Madini , Mavunde kwa kila jambo ambalo umekuwa ukiahidi unalitekeleza kwa ufanisi mkubwa ili kuweza kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye mapato, ajira na ukuzaji wa mnyororo wa thamani,” alisisitiza Dkt. Ngido.

Dkt. Melkiory Ngido aliongeza kuwa Barrick ambayo hapa nchini inaendesha shughuli zake kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga itaendelea kushirikiana na serikali katika shughuli za utafiti wa kisasa wa kijiolojia na maeneo ambayo yatakuwa hayana vigezo kwa uwekezaji mkubwa watarudisha leseni kwa serikali kwa ajili ya kupewa wachimbaji wadogo.

Dkt. Ngido pamoja na mambo mengine alichukua nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya mkoa , wilaya na viongozi wa wengine mkoani Mara kwa kuboresha mahusiano kati ya mgodi wa Barrick North Mara na vijiji vinavyozunguka mgodi huo kwani mahusiano yameleta tija kwenye ajira ,mapato ya halmashauri na maelewano kwenye jamii.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Leseni za Utafiti na Uchimbaji wa Barrick , Genes Mkumbo alisema kuwa Barrick imekuwa ikifanya shughuli za uchimbaji tangu 2020 na baada ya kuongeza nguvu Barrick ina takribani Kilometa za mraba 4,900 za leseni za utafiti ambazo inazimiliki.
“Katika mradi huu, shughuli kubwa ni kufanya utafiti wa Jiofizikia kwa kutumia Helikopta (High-Resolution airborne geophysical survey) ili tuweze kuelewa zaidi juu taarifa za miamba ya eneo hili”.

“Utafiti wa aina hii utaweka msingi Madhubuti utakaosaidia shughuli za utafiti zitakazofuatia kufanyika kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu kuvumbua maeneo mapya yenye dhahabu,” alisema Mkumbo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini , Subira Mgalu amesema kwamba programu ya kesho iliyo bora kwa sekta ya madini ni muhimu kwa kupanua wigo wa wanufaika kwa kushirikiana na Mgodi wa Barrick North Mara

Aliongeza kwamba uzinduzi wa helikopta ya kisasa ya utafiti wa kisayansi wa kijiolojia utaongeza ufanisi kwenye sekta ya madini na kuchochea ukuaji wa mnyororo wa thamani.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, alishukuru Wizara ya Madini na kampuni ya Barrick kwa namna ambavyo wameendelea kulipa msukumo suala la kuwezesha vijana kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za sekta hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, aliishukuru serikali na Mgodi wa Barrick North Mara kwa kuwezesha matukio ya kimaendeleo, ikiwemo ugawaji wa leseni kwa vikundi vya vijana wachimbaji wa madini katika eneo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, aliwapongeza wakazi wa Nyamongo kwa ushirikiano wao uliosaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa vitendo vya uvamizi kwenye eneo la Mgodi wa Barrick North Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa helikopta ya kisasa ya Barrick kwa ajili ya utafiti wa kijiolojia mkoani Mara.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akiwa katika picha ya pamoja na vijana wachimbaji wa madini wakati wa ziara yake wilayani Tarime, mkoani Mara.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akiwa katika picha ya pamoja na vijana wachimbaji wa madini wakati wa ziara yake wilayani Tarime, mkoani Mara.
Wazee wa kimila kutoka kata mbalimbali za Nyamongo wakishiriki katika hafla ya uzinduzi wa helikopta ya kisasa ya Barrick kwa ajili ya utafiti wa kijiolojia mkoani Mara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com