Na Mwandishi wetu
Watuhumiwa 36 kati ya 130 waliokamatwa kwa tuhuma za kupanga na kuhamasisha vitendo vya kihalifu wamefikishwa mahakamani, Jeshi la Polisi Tanzania limethibitisha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, DCP David Misime leo Jumapili Julai 26, 2026 watuhumiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za kuchochea na kupanga vitendo vya vurugu, kuharibu mali za umma na binafsi, kushambulia watu, pamoja na kuvuruga amani na usalama wa nchi.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni mbalimbali baada ya kubainika kuwa walihusishwa na mipango ya kuandaa na kuhamasisha vitendo vya kihalifu vilivyosababisha au vilivyolenga kusababisha uvunjifu wa amani.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa baadhi ya watuhumiwa wanadaiwa kutumia mitandao ya kijamii na njia nyingine za mawasiliano kuhamasisha mikusanyiko isiyofuata sheria, kusambaza jumbe zinazodaiwa kuwa za uchochezi, pamoja na kuratibu mipango ya vitendo vya uhalifu.
Aidha Jeshi la Polisi limesema ushahidi uliokusanywa unaonyesha kuwepo kwa tuhuma za kushiriki katika vitendo vya kuchochea vurugu, kushambulia raia, kuharibu mali na kuzuia utekelezaji wa majukumu ya vyombo vya dola.
Jeshi la Polisi pia limewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu nchini.

Social Plugin