
Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendeleza maridhiano ya kisiasa kuelekea hatua za maboresho ya katiba kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na viongozi wa vyama 18 vya siasa nchini Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo yaliyohusu maridhiano, mageuzi ya kisiasa, uchumi, huduma za jamii, ajira, uwekezaji na ulinzi wa amani, Rais Samia alirejea hatua zilizofikiwa za maandalizi ya mchakato wa maridhiano visiwani Zanzibar na kueleza kuwa serikali itaendelea kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kwa mazungumzo mara tatu kwa kila mwaka, huu ukiwa ni mkutano wa pili tangu kufanyika toka Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mkutano wa awali ulifanyika Machi 31 mwaka huu ukikutanisha wagombea urais na wenza.
Akizungumzia upande wa uchumi na maendeleo ya nchi, Rais Samia alibainisha kuwa uchumi umeendelea kukua kwa asilimia sita katika mwaka uliopita huku ukuaji wa asilimia 6.3 ukitarajiwa mwaka huu.
Alisema serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kukamilisha miradi ya maendeleo, kuendeleza uwekezaji wa miundombinu ya kimkakati kamareli, barabara, na bandari, ambapo maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam na upanuzi wa bandari za Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa vimeongeza uwezo wa kuhudumia biashara za ndani na kikanda.
Wakati wa mkutano huo uliowakutanisha wenyeviti, makamu wenyeviti, makatibu wakuu na viongozi wa jumuiya za vyama vya siasa, viongozi hao waliwasilisha maoni yao ya ustawi wa nchi, huku Rais akivitaka vyama vya siasa kulinda amani, uhuru na maslahi ya taifa kama wajibu wa pamoja, serikali ikiahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yote kupitia majukwaa stahiki ya majadiliano.









Social Plugin