Baada ya takribani miezi nane ya mgogoro uliozuka kufuatia matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 na kusababisha vurugu zilizoharibu baadhi ya majengo ya serikali na binafsi, ikiwemo madarasa ya Shule ya Msingi Idukilo, wananchi wa Kata ya Idukilo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wameomba radhi na kuahidi kuimarisha amani, umoja na mshikamano.
Vurugu hizo pia zilisababisha baadhi ya viongozi wa maeneo hayo, wakiwemo wenyeviti wa vitongoji, sungusungu na Diwani wa Kata hiyo, kukimbia maeneo yao kutokana na hali ya sintofahamu iliyokuwepo.
Wakizungumza Juni 7, 2026 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Idukilo, Wananchi wameeleza kuwa chanzo cha vurugu hizo ni kutoridhishwa kwa baadhi ya watu na matokeo ya uchaguzi huo. Hata hivyo, wamekiri kuwa mgogoro huo umewaathiri kwa kiasi kikubwa na kuwalazimu kuishi katika mazingira magumu kana kwamba ni kisiwa kisichopata huduma muhimu za kijamii na kiutawala.
Wamesema biashara zimedorora, upatikanaji wa maji safi na salama umekuwa changamoto, huku huduma za viongozi wa vijiji na kata, ikiwemo utoaji wa ushahidi unaohitajika katika shughuli za ununuzi wa ardhi, zikikosekana hali iliyosababisha maisha ya taabu kwa wananchi wengi.
Pamoja na mambo mengine, wananchi hao wameomba matumizi ya lugha nzuri na rafiki na kuondolewa kwa makundi yanayochochea mgawanyiko miongoni mwa baadhi ya viongozi na wananchi, wakisema hali hiyo imekuwa ikijenga chuki na kuendeleza migawanyiko ndani ya jamii.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, wananchi hao waliomba radhi kwa yaliyotokea na kuomba kurejeshewa huduma zote za kiserikali walizokuwa wanazikosa kutokana na mgogoro huo. Pia walieleza kushuhudia matukio mbalimbali yasiyoridhisha yakiwemo vitisho vya maisha, vitisho na kuharibiana mali kwa wote waliousika na siasa na vitendo vya kudhalilishana.
Akizungumza katika mkutano huo wa maridhiano, Diwani wa Kata ya Idukilo, Sarah Marco Mholi, amewataka wananchi kuweka pembeni tofauti zao, kusameheana na kuendelea kujenga upendo na mshikamano kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Kata hiyo.
"Maendeleo hayawezi kupatikana pasipo amani na umoja. Ni wakati wa kusameheana, kushirikiana na kuijenga upya Idukilo yetu," alisema Diwani Mholi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, amewataka wenyeviti wote wa vitongoji waliorejesha mihuri yao kuichukua na kurejea kazini mara moja ili kurejesha huduma kwa wananchi.
Amesema iwapo kiongozi yeyote atakuwa na tuhuma dhidi yake, wananchi wana haki ya kutumia taratibu za kisheria na kidemokrasia, ikiwemo kuwasilisha malalamiko yao kwa mamlaka husika na asilimia 75% ya wananchi wanaruhusiwa kumpigia kura za kumkataa.
Mhe. Masindi pia mbali na kuwataja kwa majina amewaonya vinara wanaodaiwa kuchochea vurugu hizo, akisisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayehusika na kuvuruga amani au kuzuia utendaji kazi wa serikali.
"Nataka vurugu hizi ziishe leo na zisijirudie tena. Tunafunga ukurasa na kuanza upya. Serikali ipo na inaona kila kinachoendelea. Kabla ya kufanya jambo lolote, fikiria familia yako, ndugu zako, mke na watoto wako utawaachaje endapo utachukua na kutenda hatua zinazokiuka sheria," amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Hatua hiyo ya maridhiano imepokelewa kwa matumaini makubwa na wananchi wa Idukilo, ambao sasa wanatarajia kurejea kwa huduma za msingi pamoja na kuanza upya safari ya maendeleo baada ya kipindi kirefu cha migogoro na sintofahamu.
Social Plugin