Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UFAFANUZI KUHUSU PENDEKEZO LA MHE. PROF. RIZIKI SHEMDOE LA KUWEPO KWA TRENI YA MAPEMA YA SGR KATI YA DAR ES SALAAM NA DODOMA NA KATI YA DODOMA NA DAR ES SALAAM



Dodoma, 30 Juni, 2026




Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu mjadala unaondelea katika mitandao ya kijamii kuhusu pendekezo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, alilolitoa la kuomba kuanzishwa kwa huduma ya treni ya SGR ya mapema sana alfajiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma, ambalo limetafsiriwa tofauti na ilivyokusudiwa.




Mhe. Prof. Shemdoe alitoa pendekezo hilo wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi katika hafla ya kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa 2026, wakati alipotembelea banda la Wizara ya Uchukuzi, ambapo alieleza changamoto ya uwepo wa mahitaji ya wananchi ya huduma ya treni ya mapema alfajiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.




Lengo la pendekezo hilo lilikuwa ni kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi wote wenye mahitaji ya kufika mapema katika miji hiyo miwili kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo kuhudhuria mikutano, kupata huduma za Serikali na binafsi, kufanya biashara, kuhudhuria matibabu, masomo na shughuli nyingine. Mheshimiwa Waziri alitoa mfano wa watumishi wa umma ambao wenza wao wanafanya kazi katika miji tofauti, hususan pale ambapo taasisi zao hazina ofisi katika mji mmojawapo. Alieleza kuwa huduma hiyo ingeweza kuwasaidia watu wa aina hiyo pamoja na makundi mengine mengi ya wasafiri kurejea mapema kwenye maeneo yao ya kazibaada ya mapumziko ya mwisho wa wiki. Mfano huo ulikuwa ni sehemu ya kuelezea uhitaji uliopo na haukuwa na lengo mahususi la kuwawezesha watumishi wa umma pekee.




Huduma za usafiri wa treni kwa safari za mapema katika ya miji mikubwa ni jambo la kawaida katika nchi nyingi zenye mifumo ya kisasa ya reli. Hivyo Tanzania hivi sasa ni mojawapo ya nchi zenye reli ya kisasa kupitia uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo inaendelea kupanua fursa za usafiri salama, wa haraka na mapema wenye kuzingatia mahitaji ya wananchi.




Kwa mantiki hiyo, ni vyema kauli ya Mheshimiwa Waziri ikaeleweka katika muktadha wake halisi wa kuboresha huduma za usafiri kwa manufaa ya wananchi wote, badala ya kutafsiriwa kuwa inalenga kundi la watumishi wa umma.




Aidha wananchi mnaombwa kuipokea hoja hiyo kwa kuzingatia maudhui yake halisi na kupuuza tafsiri zinazopotosha kusudio la pendekezo hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com