NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Serikali imesema mafanikio yaliyofikiwa na kiwanda cha kuunganisha magari aina ya Howo kinachomilikiwa na Saturn Corporation Limited ndani ya kipindi cha miaka miwili ni ushahidi wa ukuaji wa sekta ya viwanda nchini, huku uzalishaji, ajira na mapato ya Serikali vikiongezeka kwa kasi.
Akizungumza leo Mei 24, 2026 wakati akiweka jiwe la msingi la kiwanda kipya cha kutengeneza magari madogo ya mizigo aina ya pick-up, cha kampuni hiyo Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 65 umewezesha kiwanda hicho kuongeza uwezo wa kuunganisha magari kutoka magari 10 kwa siku wakati wa uzinduzi wake mwaka 2024 hadi magari 30 kwa siku kwa sasa.
Kapinga amesema ongezeko hilo linaakisi imani ya wawekezaji kwa uchumi wa Tanzania na mafanikio ya jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia sera rafiki, uboreshaji wa miundombinu ya uzalishaji pamoja na mifumo wezeshi ya biashara.
Amesema Serikali ina matarajio ya kuona kiwanda hicho kikifikia uwezo wa kuunganisha magari 100 kwa siku katika siku zijazo, hatua itakayosaidia kuongeza ajira, kukuza teknolojia ya uzalishaji wa magari, kuongeza mapato ya Serikali na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa magari katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katika maadhimisho hayo, Waziri Kapinga pia alishuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda kipya cha kutengeneza magari madogo ya mizigo aina ya pick-up, hatua iliyotajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kupanua uzalishaji wa magari nchini na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa magari kutoka nje.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi huo mpya unatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa magari, kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana, kuimarisha ujuzi wa teknolojia ya magari na kuibua fursa za biashara kwa wazalishaji wa vipuri pamoja na watoa huduma mbalimbali ndani ya sekta ya magari.
Katika kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake, kiwanda hicho kimezalisha zaidi ya magari 5,000 yaliyosambazwa katika soko la ndani na nje ya nchi, jambo ambalo Serikali imelielezea kuwa ishara ya ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na ushindani wake katika soko la kimataifa.
Aidha, Kapinga amesema ajira za moja kwa moja zimeongezeka kutoka wafanyakazi 155 wakati wa uzinduzi hadi zaidi ya wafanyakazi 360 wote wakiwa Watanzania, huku zaidi ya ajira 2,500 zisizo za moja kwa moja zikichangiwa na shughuli mbalimbali zinazohusiana na uzalishaji wa magari.
Kuhusu mchango wa kiwanda hicho kwa uchumi, amesema ndani ya miaka miwili ya uendeshaji wake, Saturn Corporation imechangia zaidi ya Shilingi bilioni 40.7 kwa Serikali Kuu na Shilingi bilioni 1.5 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni kupitia kodi na tozo mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Saturn Corporation, Rehmatullah Habib amesema wengi wa vijana walioajiriwa wamepatiwa mafunzo ya uunganishaji wa magari, uhandisi na uzalishaji viwandani, hatua iliyowezesha Watanzania kuendesha kwa ufanisi mifumo ya kisasa ya uunganishaji wa magari ambayo hapo awali ilitegemea kwa kiwango kikubwa utaalamu wa kigeni.
“Mbali na ajira za moja kwa moja, kuna wanufaika wengi wanaotegemea shughuli za kampuni hii kwa njia isiyo ya moja kwa moja, wakiwemo wafanyabiashara wa maeneo jirani, wasafirishaji na wengine wanaohusika katika mnyororo wa huduma za kampuni,” amesema Habib.
Social Plugin