Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA YATOA WITO WA UTAWALA BORA KUIMARISHA UWEKEZAJI WA UMMA

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Chacha Marigiri, akiwasilisha mada kuhusu ‘Utawala bora katika mashirika ya Umma na Majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina’  katika Mkutano wa Jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma Zanzibar uliofanyika tarehe 24 Mei 2026 katika hoteli ya Golden Tulip Airport.

**

Zanzibar. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imesisitiza kuwa mustakabali wa mafanikio ya taasisi na mashirika ya umma nchini unategemea kwa kiwango kikubwa uimara wa mifumo ya utawala bora, uwajibikaji na uongozi wenye maono yanayolenga matokeo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Chacha Marigiri, alipowasilisha mada kuhusu ‘Utawala bora katika mashirika ya Umma na Majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina’  katika Mkutano wa Jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma Zanzibar uliofanyika katika hoteli ya Golden Tulip Airport.

Katika wasilisho lake Jumapili, Mei 24, 2026, Bw. Marigiri alisema kuwa kasi ya kufikia maendeleo endelevu haiwezi kupatikana kwa uwekezaji pekee, bali kupitia mifumo imara ya usimamizi inayohakikisha rasilimali za umma zinalindwa na kuzalisha kwa maendeleo ya Taifa.

Alisema thamani ya uwekezaji wa Serikali katika taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache kwa sasa imefikia Sh92.3 trilioni, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya utawala bora na usimamizi wa uwekezaji wa umma.

Kwa sasa Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia uwekezaji wa umma wenye jumla ya taasisi 308, zikijumuisha taasisi za kibiashara, zisizo za kibiashara pamoja na uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Hali hiyo inaifanya OMH kuwa mhimili muhimu katika kulinda na kuongeza thamani ya mali za Serikali.

Bw. Marigiri alisema jukumu la OMH linaenda zaidi ya usimamizi wa kawaida mpaka kuhakikisha taasisi za umma zinaendeshwa kwa nidhamu ya kifedha, zinakuwa na ufanisi wa kiutendaji na zinaendana na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Alitaja maeneo muhimu ya mamlaka na majukumu ya OMH kuwa ni pamoja na kusimamia utendaji wa taasisi za umma, kufuatilia faida na marejesho ya Serikali kupitia gawio, kushauri kuhusu uteuzi na tathmini ya bodi, kufanya tathmini ya utendaji pamoja na kushauri Serikali kuhusu maamuzi ya uwekezaji.

Katika hatua nyingine, aliwataka wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu kuendelea kuimarisha mifumo ya utawala kwenye taasisi zao kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia, usimamizi wa vihatarishi, usimamizi wa maadili pamoja na maamuzi inayozingatia takwimu.

Alisema uzoefu wa mataifa yaliyofanikiwa kiuchumi kama Singapore, Norway, China na Malaysia unaonesha kuwa mafanikio ya uwekezaji wa umma yanategemea zaidi ubora wa usimamizi kuliko ukubwa wa uwekezaji wenyewe.

“Taifa lolote halifanikiwi kwa kumiliki taasisi za umma pekee; mafanikio yanatokana na namna taasisi hizo zinavyosimamiwa kwa weledi, uwajibikaji na malengo muda mrefu,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa OMH imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (2025/26–2049/50) unaolenga kuifanya ofisi hiyo kuwa kichocheo cha upanuzi wa uchumi kupitia uwekezaji wa Serikali na hasa katika sekta za kimkakati ikiwemo usafirishaji, nishati, fedha, kilimo, viwanda, utalii na madini.

Alisema mafanikio ya uwekezaji wa umma yataendelea kutegemea ushirikiano wa karibu kati ya bodi za taasisi, watendaji wakuu, Serikali na taasisi za usimamizi ili kujenga taasisi imara, zenye ushindani na zinazotoa matokeo yanayopimika kwa maendeleo ya Taifa.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com