Video: TUNDU LISSU ASIMULIA KILA KITU TANGU APIGWE RISASI, KESHO KUSAFIRISHWA KWENDA NJE YA KENYA


Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu amefunguka na kusema kuwa kesho Januari 6, 2018 atasafiri na kutoka nje ya Kenya kwenda kufanyiwa matibabu zaidi kufuatia shambulio la kupigwa risasi lililotokea mwaka jana.


Lissu amesema hayo leo wakati akiongea na waandishi wa habari akiwa nje ya hospitali ya Nairobi na kusema kuwa amekuwepo hapo kwa takribani miezi minne akifanyiwa matibabu lakini sasa anakwenda kufanyiwa matibabu zaidi sehemu nyingine.


Mbali na hilo Tundu Lissu ameendelea kusema kuwa shambulio lake kupigwa risasi ni tukio la kisiasa ndiyo maana viongozi wa bunge wamekuwa wakishikwa na kigugumizi.


Amesema Bunge limeshindwa kumhudumia na kumlipia matibabu kama ambavyo inapaswa kuwa lakini pia hakuna kiongozi yoyote wa Bunge ambaye amethubutu hata kwenda kumuona.


"Leo nazungumza Bunge la Tanzania halijatoa hata shilingi moja wakati sheria ipo wazi, ndugu zangu wamewaandikia barua ya kuwaomba kupata haki ya matibabu lakini mpaka tunazungumza sasa hivi Spika wa Bunge, Naibu Spika wa Bunge, Katibu wa Bunge wala hakuna kiongozi wowote wa Bunge aliyefika kuniona kwa miezi hii minne, walijua sitaweza kupona ndiyo maana hawakuwa na Plan ya kunitibu" amesema Lissu


Aidha Mbunge huyo ametoa maoni yake kuwa anaamini jaribio la yeye kutaka kuuawa mnamo Septemba 7, 2017 ni jaribio la kisiasa na amedai anaamini jeshi la polisi nchini Tanzania hawapelelezi juu ya tukio hilo.


"Maoni yangu kilichofanyika kilikuwa ni jaribu ya mauaji ya kisiasa moja kwa moja, mimi siyo mfanyabiashara, jeshi la polisi kwa maoni yangu hawapelelezi tukio hili kwa sababu sijawahi ona mtu anakuja kuniuliza, wanamtaka dereva wangu kwaajili ya kumkamata na sio kumhoji juu ya tukio hilo" amesema Tundu Lissu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527