RAIS MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA MASOKO YA AFRIKA KAMPUNI YA UTENGENEZAJI NDEGE YA BOEING


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 05 Desemba, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao yake nchini Marekani Bw. Jim Deboo ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kununua ndege kubwa kutoka kampuni hiyo.


Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James.


Baada ya Mazungumzo hayo Rais Magufuli amesema Serikali yake ya Awamu ya Tano imedhamiria kununua ndege nyingine nne zikiwemo ndege kubwa 3 ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja hapa nchini moja kwa moja kutoka nchi zao.


"Sisi hapa tunazungumza kuwa watalii hawajafika hata milioni 2 kwa mwaka, lakini nchi kama Morocco inapata watalii zaidi ya milioni 12 kwa mwaka, hii yote ni kwa sababu hatuna mashirika ya ndege ya kwetu, watalii wakitaka kuja hapa ni lazima waje kwa kuungaunga, wafikie nchi nyingine halafu ndipo wapate moyo wa kuja huku, licha ya kwamba sisi Tanzania ni miongoni mwa nchi 5 duniani zenye maeneo mazuri yenye utalii.


"Kwa hiyo niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati mwingine nikiangalia mitandao na magazeti ni ajabu huwezi kuamini kama hao ni Watanzania, unakuta wanasifia tu ndege za watu wengine na wanazibeza za kwao" amesisitiza Rais Magufuli.


Mhe. Rais Magufuli ametaja aina ya ndege mpya ambazo Serikali itazinunua kuwa ni ndege 1 aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kufika nchini Mwezi Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018 na ndege moja aina ya Boeing 787 Dash 8 Dream Liner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 na inayotarajiwa kuwasili nchini Juni, 2018. Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika.


Dkt. Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi za Serikali zenye lengo la kuinua utalii na kuimarisha uchumi wa nchi.


"Tumeleta ndege aina ya Bombardier hapa, zimepunguza gharama za safari mfano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, sasa wanalipa kati ya 160,000/ hadi 200,000/- wakati nauli ilishafika Shilingi laki 8 na kitu, lakini watu wengine utakuta wanazungumzazungumza wee maneno ya hovyo kwa kutumiwa, tumeshaamua na tutafanya hivyo" amesisitiza Rais Magufuli.


Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagana na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika hapa nchini (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero ambaye amepandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Ukanda wa Kusini mwa Afrika katika ofisi zake zilizopo Afrika Kusini.


Rais Magufuli amemshukuru Dkt. Tonia Kandiero kwa juhudi kubwa alizozifanya akiwa Mwakilishi Mkazi wa AfDB hapa nchini ambapo miradi mikubwa na muhimu katika maendeleo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa.


Akizungumza baada ya kuagana na Rais Magufuli Dkt. Tonia Kandiero amemshukuru Rais Magufuli na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano alioupata katika kipindi cha miaka 6 aliyokuwa hapa nchini na amesema anaondoka akiwa ameiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa ya kimahusiano na AfDB ambapo miradi yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 2 imetekelezwa hususani katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.


Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo anayemaliza muda wake baada ya kuiwakilisha nchi ya Cuba kwa miaka minne.


Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo kwa uhusiano na ushirikiano mzuri aliouendeleza kati ya Tanzania na Cuba uliojengwa na waasisi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mhe. Fidel Castro wa Cuba


Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo amemshukuru Rais Magufuli na Serikali kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Cuba na amesema anaondoka akiwa anaamini kuwa uhusiano kati ya nchi hizi utaendelea kuwanufaisha wananchi ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo na huduma za kijamii.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Desemba, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitazama kitabu cha picha ya ndege aina ya Boeing 787-8 Dream liner wakati alipokuwa akisikiliza maelezo yake kutoka kwa Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo. Ndege hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 262 na itakuwa na uwezo wa kuruka kutoka nchini Marekani hadi Tanzania bila kutua mahali popote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Cuba anayemaliza muda wake hapa nchini George Luis Lopez Tormo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo. Dkt. Tonia ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Ukanda wa Kusini Mwa Afrika katika Ofisi zake zilizopo Afrika ya Kusini

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527