Ushirikina Katavi: NYUMBA ZAPAKWA DAMU NA WATU WASIOJULIKANA USIKU

Wakazi wa Kata ya Nsemlwa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi wanalazimika kulala mapema kutoka na kushikwa na hofu baada ya nyumba zao wanazoishi kukutwa zimepatwa damu ikiwemo ofisi ya mtendaji wa kata hiyo damu ambayo haija julikana ni ya binadamu au ya mnyama nje ya nyumba zao na ndani ya nyumba.

Afisa mtendaji wa kata ya Nsemlwa Jumbe Mselwa aliwaambia wandishi wa Habari jana kuwa tukio hilo la watu kukuta nyumba zao zimepakwa damu na watu wasiofahamika limetokea usiku wa kuamkia Juma pili na usiku wa kuamkia jana hivyo kujenga hofu kubwa kwa wakazi wa kata hiyo.

Alisema tukio hilo la wakazi wa kata hiyo nyumba zao kupakwa damu usiku na watu wasiojulikana limetokea kwenye mitaa yake yote mitano ambapo taarifa hizo zilifikishwa ofisini kwake na wenyeviti wa wa mitaa hiyo mitano na baada ya kupata taarifa hizo alilazimika kwenda kuhakikisha na kukuta nyumba hizo zikiwa zimepakwa damu nje na nyingine ndani ya nyumba .

Jumbe aliitaja mitaa hiyo ambayo nyumba zake zimepakwa damu kuwa ni Mtaa Kichangani , Migazini ,Kilimani Tulieni na Mtaa wa Nsenlwa ambao ndio unaongozwa kwa nyumba nyingi kupakwa damu .

Alisema kutokana  na hali hiyo,   amewataka wakazi wa kata hiyo mara wanaopoona kitu ambacho sio cha kawaida watoe taarifa na mapema kwa uongozi wao wa mitaa wanayoishi .

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nsemlwa Adamu Masigati alisema nyumba yake ni miongoni mwa nyumba ambazo zimepakwa damu na yeye na wananchi wa Mtaa huo wamekuwa wakijiuliza kwanini tukio hilo linatokea usiku badala ya mchana .

Akisimulia mkasa huo mmoja wa wananchi waliopatwa na mkasa huo, Raphael Geoge alisema juzi alikuwa nyumbani kwake majira ya saa kumi jioni akila chakula ugali sebuleni kwake,lakini aliposhika tonge la pili ghafla aliona matone mawili ya damu yakidondoka chini alipokuwa amekaa.

Alisema hali hiyo ilimshitua na kumfanya amwite mtoto wake wa kike anaitwa Maliselina Joseph ili nae ashuhudie damu hiyo ambayo haikufahamika imetoka wapi na ni ya mnyama gani.

Majirani wa eneo hilo walifika nyumbani kwa Raphael na kujaa kwa wingi na walishtushwa na hali hiyo na hasa baada ya kuona inzi wamejaa kwenye damu hiyo na ndipo walipokwenda kutoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya mtaa.

Mkewe Raphael aitwaye Judith Joseph ambae wakati wa tukio hilo hakuwepo nyumbani aliporudi nyumbani majira ya saa moja na nusu usiku alikuta familia yake wakiwa wamekaa kama wagonjwa.

Alisema hali hiyo ilimshtua sana na ndipo alipopewa maelezo na mme wake juu ya tukio hilo na ndipo alipomshauri mme wake kuwa wahame kwenye nyumba hiyo hata hivyo mume wake alikataa kwa kile alichodai kuwa ingekuwa ni nyumba ya kupanga wangehama .

Judith alieleza kuwa kutokana na tukio hilo ana siku mbili sasa ameshindwa kufanya usafi wa nyumba kutokana na hali ya hofu na pia tangu   siku hiyo wanalazimika yeye na familia yake kulala mapema muda wa saa mbili usiku .

Nae Wastala Ferusi alisema yeye na familia yake tangu  nyumba yao ilipopakwa damu wamekuwa wakijifungia na kulala mapema na amekuwa akiwakataza watoto wake kutembea hata kwa majirani.

Alisema tatizo la tukio hilo ni kwamba kama damu haikupakwa nje basi ujue imepakwa ndani ya nyumba.

Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527